NA GODFREY NNKO
ZAIDI ya washiriki 1,000 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi ndani na nje ya nchi wamethibitisha kushiriki katika uzinduzi wa Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Washiriki hao wanajumuisha vyama,Bodi za Kitaaluma, Balozi zaidi ya 20, taasisi za kimataifa 10, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Wenyeviti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mawaziri, Mhimili wa Mahakama, taasisi za fedha na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi.
Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Bw.Muungano Saguya ameyabainisha hayo leo Novemba 11,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
"Kumekuwa na utayari mkubwa wa makampuni na taasisi binafsi za nje na ndani ya nchi kutaka kuwekeza katika ujenzi wa majengo makubwa kwenye viwanja vya NHC.
"Kutokana na hali hiyo, shirika limeona ni vema kuchambua na kuainisha zaidi maeneo ya kutosha ya kukidhi shauku hiyo ya kujenga nchi yetu. Hapo awali tulitenga maeneo 60 tu yenye viwanja au majengo yanayohitaji kuendelezwa.
"Kwa msukumo uliopo sasa tumeamua kuongeza maeneo zaidi ili yaendelezwe.
"Ili kutoa muda wa kuchambua na kuidhinisha maeneo hayo mapya yatakayotangazwa wakati wa mkutano wa uzinduzi, Shirika la Nyumba la Taifa limeamua kusogeza mbele uzinduzi huo hadi Jumatano ya tarehe 16 Novemba 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam,"amefafanua Saguya.
Katika uzinduzi huo,Saguya amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb).
"Mkutano utaanza saa mbili kamili asubuhi. Tunawaomba wananchi na wageni waalikwa wawe wamefika majira ya saa 1.30 asubuhi na kwa wale ambao hawatabahatika kuwapo ukumbini, uzinduzi huo utaoneshwa mubashara na vituo vya televisheni vya ITV, TBC1, vyombo vya habari vya ahirika na pia tutakuwa na link ya zoom kwa washiriki wa nje kuweza kufuatilia.
"Shirika linatayarisha vitabu maalumu viwili vinavyoelezea sera hiyo ya ubia na maeneo ya uwekezaji ya NHC yalipo, yakielezea taarifa zote muhimu kwa kina. Tunachukua fursa hii kuwakaribisha wawekezaji na wadau muhimu siku hiyo ya tarehe 16 Novemba.
"Tumejipanga vema siku hiyo ya uzinduzi ambapo kutakuwa na vyumba 12 vilivyoandaliwa kupokea maoni ya wawekezaji na kuwapa maelezo watakaohitaji.
"Naomba nisisitize kuwa hakuna haja ya kuwa na dalali au mtu wa kati ili mwekezaji kupata fursa ya kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa kujenga majengo kwa ubia. Sera hii ipo wazi na ina vigezo na masharti ya kuzingatiwa na kila anayehitaji na haihitaji kujuana na mtu yeyote wa NHC ili kupata mradi,"amefafanua Saguya.
Meneja huyo amefafanua kuwa,uzinduzi wa Sera ya Ubia unaenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na wanaunga mkono maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kuleta na kujenga uchumi wa Taifa letu.
Pia amesema,Sera ya Ubia iliyoboreshwa imezingatia maslahi ya wabia, Shirika la Nyumba la Taifa na Taifa kwa ujumla.
Sera ya ubia ambayo NHC inawaalika Wawekezaji kushiriki ilianzishwa na Shirika tangu mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika.
Aidha, maboresho ya mwisho yamefanyika mwaka 2022 ili kuondoa changamoto zilizojitokeza hapo awali.
"Tangu kuanza kwa utaratibu huu, jumla ya miradi 111 ilitekelezwa ikiwa na thamani ya shilingi Bilioni 300. Katika miradi hiyo, miradi 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 240 imekamilika na kuanza kutumika na miradi 30 yenye thamani ya shilingi Bilioni 60 inaendelea kukamilishwa,"amebainisha Saguya.