Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yakabidhi msaada kwa watoto waliopo kwenye vizuizi vya kisheria

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Mashtaka Tanzania, Bw Sylvester Mwakitalu, amekabidhi msaada wa magodoro, taulo za kike, mashuka, mafuta na sabuni kwa Mkuu wa Gereza la mahabusu Segerea,Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamisi Lissu.
Mkurugenzi Mwakitalu amesema msaada huo pamoja na vitu vingine umetolewa kwa ajili ya kuwahudumia watoto ambao wameshikiliwa kwenye vizuizi vya kisheria kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya.

Msaada huo uliwasilishwa baada ya kuupokea kutoka Shirika la Utangazaji (TBC) ambalo lilitoa msaada huo kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni mchango wa shirika hilo katika kuisaidia jamii.

"Nashukuru wadau wote wanaoendelea kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya uhalifu na leo asubuhi nimepokea msaada wa magodoro, mashuka, taulo za kike, sabuni na mafuta kutoka Menejiment ya Shirika la Utangazaji Nchini (TBC) kwa ajili ya kuwapelekea watoto waliopo vizuizini na waliokinzana na sheria,"amesema Mkurugenzi Mwakitalu.
"Tunalo kundi kubwa la watoto ambao wanakaa kwenye Magereza na wazazi wao ( wanawake) ambao wanapatikana na hatia au wameshtakiwa kwa makosa ya jinai kwa sababu moja au nyingine anakosa dhamana na kwenda gerezani wakiwa na watoto wao na hawa ndio kundi kubwa ambalo lipo katika Magereza yetu," amesema Mwakitalu.

Akimkabidhi msaada huo kwa DPP, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Moses Chitama, amesema msaada huo unalenga kurudisha fadhila kwa jamii, hivyo alitoa wito kwa jamii na wadau mbalimbili ikiwemo Sekta binafsi na mashirika ya umma kuiga mfano kwa TBC wa kusaidia jamii.

Chitama amesema, msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 5 umetolewa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwenda ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa ajili ya kuupeleka gerezani kwa watoto wa wenye uhitaji maalumu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Segerea, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamis Lissu, amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kutokana na watoto kuhitaji misaada mbalimbali ikiwemo magodoro na sabuni na vitu vingine.
"Msaada huu utaenda kutumika kama ulivyokusudiwa kwa walengwa, hivyo tunaomba wadau wengine waige mfano kama huu ulioonyeshwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Shirika la Utangazaji nchini kwa kuwa kuwajali wahitaji," amesema SSP Lissu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news