NA FRESHA KINASA
KATIKA kuendelea kulinda mazingira na uoto wa asili Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof.Sospeter Muhongo amesema, yupo tayari kuanza zoezi la usambazaji wa miche ya miti 100,000 ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.
Mheshimiwa Prof. Muhongo ameyasema hayo leo Novemba 30, 2022 kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Mara (RCC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Mjini Musoma.
Amesema, ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira miche ya miti hiyo ya aina mbalimbali itasambazwa bure kwa wananchi pamoja na taasisi za umma na binafsi ili kuweza kuendelea kuyatunza mazingira yaweze kuendelea kuwa bora na kuwaneemesha wananchi kwa kupata faida mbalimbali.
Mheshimiwa Muhongo ameongeza kuwa, katika kipindi cha nyuma alishasambaza miche ya miti 10,000 na jitihada bado zinaendelea kusambaza miche hiyo ya miti katika Jimbo la Musoma Vijijini ili iweze kupandwa.
Ameongeza kuwa, siku zote anapenda kufanya kazi kwa vitendo na miche ya miti 100,000 ipo tayari na katika msimu wa mvua itasambazwa ili ipamdwe na zoezi hilo litakuwa endelevu jimboni humo.
Akizungumzia maendeleo ya Mkoa wa Mara, Prof. Muhongo amesema ili kuendelea kiuchumi na mkoa huo uzidi kupaa kimaendeleo ofisi ya mkuu wa mkoa inapaswa kushirikiana na ofisi za wakuu wa wilaya ili kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaaa ya wana Mara.
Amesema, mapato ya Mkoa wa Mara ya sasa hayawezi kuinua uchumi wa mkoa wa Mara bila kuwa na shughuli za kiuchumi zinazotokana na kilimo, uvuvi na ufugaji pamoja na uanzishwaji wa viwanda vitakavyokuwa chachu ya maendeleo jimboni humo.
Pia,Prof. Muhongo amesema katika kilimo, bonde la Bugwema likitumika kwa kilimo cha umwagiliaji kitaleta viwanda vya mazao vitakavyoinua uchumi wa mkoa wa Mara.
Katika sekta ya uvuvi, Prof.Muhongo amekiomba kikao cha RCC kufuatilia uvuvi wa vizimba ikiwa ni pamoja na kupata mikopo bila riba nafuu ambayo vitakuza uchumi kupitia uvuvi na rasilimali hizo kuweza kuwaneesha wananchi.