Rais Dkt.Mwinyi aishukuru Wizara ya Ulinzi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kuanza kushughulikia migogoro ya ardhi inayolikabili Jeshi la Wananchi Tanzania, hapa Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe.Innocent Bashungwa (Mb) alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha. (Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi ametoa shukurani hizo Novemba 11, 2022 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa (Mb) aliyefika kwa ajili ya utambulisho.

Amesema, kumekuwepo changamoto za migogoro ya ardhi inayolihusisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na raia, hali iliyosababishwa na ongezeko la makaazi ya wa wananchi katika maeneo ya migogoro.

Dkt.Mwinyi amesema amefurahishwa na juhudi zilizoanza kuchukuliwa na wizara hiyo katika kuitafutia ufumbuzi migogoro hiyo, huku akibainisha matumaini yake kuwa itamalizika vyema.

Aidha, amemhakikishia Waziri huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itampa kila aina ya ushirikiano ili kufanikisha majukumu ya kiulinzi.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumkabidhi jukumu la kuiongoza wizara hiyo, pamoja na kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapunduzi, Dkt.Hussein Mwinyi kwa kuweka misingi bora katika wizara.

Waziri Bashungwa ameahidi kuendelea kumsaidia Amiri Jeshi Mkuu katika ulinzi wa mipaka pamoja na kudumisha Muungano wa Tanzania.

Amesema, wizara yake iko mbioni kuitafutia ufumbuzi migogoro ya ardhi inayolikabili Jeshi la Wananchi wa Tanzania hapa Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news