NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS) kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanya kazi ya kuielimisha jamii dhana na dhamira ya Uchumi wa Buluu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akifuatana na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,pamoja na viongozi wa chuo hicho katika maandamano ya duru ya nne ya mahafali ya 52,yaliyofanyika leo,katika viwanja vya Taasisi ya Sayansi ya Bahari,Buyu Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.(Picha na Ikulu).
Dkt.Mwinyi ametoa wito huko Buyu Mkoa Mjini Magharibi alipozungumza katika Mahafali ya 52 Duru ya nne, ya Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Kampasi ya Buyu.
Akizungumza na wahitimu,viongozi wa chuo pamoja na wananchi, Dkt.Mwinyi amesema kuna umuhimu wa uongozi wa chuo hicho kushirkiana na Serikali na kufanya kazi ya ziada ya kuielimisha jamii juu ya dhana ya Uchumi wa Buluu na dhamira ya Serikali ya kuweka kipaumbele katika matumizi ya rasilimali za Bahari katika kuimarisha uchumi.
Amesema, Serikali itaendeleea kutoa ushirikiano na IMS katika kuimarisha Sekta ya Uchumi wa Buluu unaozihusisha sekta za uvuvi pamoja na kilimo cha mwani kwa kuamini kuwa chuo hicho ni chanzo muhimu katika kuibua watalamu.
Aidha, Dkt.Mwinyi amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa taasisi za elimu ya juu nchini na kubainisha uwepo wa IMS kuwa ni fursa muhimu katika maendeleo ya sekta ya uchumi wa buluu.
Amesema, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa IMS katika uimarishaji wa zao la mwani, lenye kuzalisha ajira kwa kiwango kikubwa, hususani kwa akinamama.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) alipokuwa akimkabidhi cheti, Kulwa Mtaki,mara baada ya kutunukiwa Digirii ya Udaktari wa falsafa katika sayansi ya za Bahari (Doctor of Philosophy in Marine Sciences) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam katika sherehe za mahafali ya 52,duru nya nne ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Taasisi ya Sayansi ya Bahari,Buyu Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.
Aliuahidi uongozi wa chuo hicho kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaifanyia matengenezo kwa kuijumuisha barabara chakavu iendayo Chuoni huko kupitia mradi wa ujenzi wa barabara za ndani unaotekelezwa na Serikali.
Aidha, ametoa maelekezo kwa Wizara ya Ardhi,Makaazi na Maendeleo kushuhulikia upatikanaji wa hatimiliki ya chuo hicho.
Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa wahitimu hao kutotosheka na kiwango cha elimu walichofikia na badala yake kutumia taaluma na maarifa waliyopata ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Naye, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akihitimisha mahafali hayo amesema, tangu mwaka 2019 Kampasi ya Buyu ilianza kuchukua wanafunzi wa shahada ya awali na hivyo kuingia katika utaratibu wa kufanya mahafali kuanzia mwaka huu, lengo likiwa ni kutangaza shughuli za chuo hicho pamoja na kuwahamasisha vijana wanaomaliza masomo ya kidato cha sita kujiunga na chuo kwa masomo ya Chuo Kikuu.
Amemshukuru Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa ahadi ya kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo hicho, ikiwemo uchakavu wa barabara, hatua itakayorahisisha safari za wanafunzi wafanyakazi kutoka hosteli hadi chuoni.
Dkt.Kikwete alisema chuo hicho kimepanga kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) kwa maslahi ya Taifa, na akabainisha azma ya chuo hicho ya kuandaa kongamano kubwa la Kimataifa litakalowashishirikisha wataalamu wabobezi kuhusu Uchumi wa Buluu ili wananchi waweze kufahamu dhana nzima ya Uchumi wa Buluu.
Baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Taasisi ya Sayansi ya Bahari,Buyu Wilaya ya Magharibi "B" Unguja wakiwa katika maandamano ya duru ya nne ya mahafali ya 52,yaliyofanyika leo,katika viwanja vya Chuo,ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani).
Mapema, Makamu Mkuu wa Chuo Prof.William A.L. Anangisye amesema, katika kuunga mkono juhudi na Dira ya Serikali zote mbili katika kuendeleza Uchumi wa Buluu kwa kutoa wataalamu wa kujenga uwezo wa kitaasisi, IMS imejizatiti katika utoaji wa mafunzo ya utafiti ili kuchochea kasi ya matumizi endelevu ya bahari yatakayotoa mchango chanya katika uchumi wa nchi na maendeleo ya kijamii.
Amesema taasisi ina mpango wa kulifanya jengo la Mizingani kuwa kituo Bobevu cha utafiti wa masuala ya Uvuvi, ikiwa ni mwendelezo wa juhudi zinazoendelea kwenye kituo cha utafiti kilichopo Pangani Tanga kinachojishughulisha na utafiti wa mbegu na chakula bora kwa ajili ya ufugaji wa samaki.
Wahitimu wa Digirii za Uzamivu,Umahiri na Awali wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa hutuba yake katika sherehe ya kuwatunuku Shahada wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Taasisi ya Sayansi ya Bahari hafla iliyofanyika leo katika viwanja vya Taasisi hiyo Buyu Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.
Amesema, kwa muda wote huo chuo kinajivunia mafanikio makubwa yaliopatikana, ikiwemo uanzishwaji na uendelezwaji wa kilimo cha mwani ambacho kimeenea kote nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji wa mwani.
Aidha, amesema IMS imefanikiwa kuanzisha utafiti mkubwa wa uzalishaji wa mbegu bora za samaki, ambapo kwa kuanzia kilianza na samaki aina ya Perege, Kolekole pamoja na Majongoo bahari.
Ameeleza kuwa, mafanikio ya wahitimu yametokana na michango iliyotolewa kwa nyakati tofauti na wadau ikiwemo serikali zote mbili, mashirka kutoka nchi rafiki, asasi za kiraia, wafadhili pamoja na familia.
Hata hivyo, amesema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya uchakavu wa barabara inayoelekea chuoni.
Prof.Anangisye amewataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kama ushawishi kwa wadau wote wanaowazunguka na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, kwa kufahamu kuwa elimu hiyo ni mali ya umma.
Baadhi ya wanafamilia wa Wahitimu wa Digirii za Uzamivu,Umahiri na Awali,wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa hutuba yake katika sherehe ya kuwatunuku Shahada wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Taasisi ya Sayansi ya Bahari hafla iliyofanyika leo katika viwanja vya Taasisi hiyo Buyu Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.
Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Sanare Maajar amesema ni matarajio ya baraza hilo kuwu wahitimu hao watakuwa chachu katika kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali za Uchumi wa Buluu, kwa kuongeza uwezo na ufanisi wa kitaasisi, uwezo wa kujiajiri kupitia taaluma na maarifa waliyopata.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mhe.Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) akimtunuku Mbiru Moses,Digirii ya Udaktari wa falsafa katika sayansi ya za Bahari (Doctor of Philosopony in Marine Sciences) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika sherehe za mahafali ya 52,duru nya nne ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,yaliyofanyika leo viwanja vya Taasisi ya Sayansi ya Bahari,Buyu Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.(kushoto) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi,akiwa mgeni rasmi wa mahfali hayo.
Wahitimu wa Digirii za Uzamivu,Umahiri na Awali wakila kiapo cha mara baada ya kutunu kiwa shahada zao leo katika sherehe za mahafali ya 52,duru nya nne ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,yaliyofanyika leo viwanja vya Taasisi ya Sayansi ya Bahari,Buyu Wilaya ya Magharibi "B" Unguja,mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani).
Amesema Baraza la Chuo linafarijika na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Uongozi wa Chuo pamoja na Serikali katika kuboresha miundombinu katika taasisi hiyo ya IMS ikiwemo ujenzi wa majengo mbalimbali pamoja na Bweni la Wanafunzi kupitia mradi wa HEET, unaokwenda sambamba na ukarabati wa jengo la Mizingani lililoathiriwa kwa kiwango kikubwa na ajali ya moto.
Mahafali ya 52 Duru ya nne yamewahusisha wahitimu 38, kati yao wahitimu wanne wa Shahada ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Bahari, wahitimu saba wa Shahada ya Umahiri wa Sayansi katika Sayansi ya Bahari pamoja na wahitimu 27 wa Shahada ya Awali ya sayansi za Bahari.