NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema uhifadhi wa mazingira ya bahari unapaswa kufanyika hatua kwa hatua kwa kuwawezesha wananchi ili kupunguza umaskini na kuleta usawa wa kijamii.
Washiriki wa Mkutano wa "7TH Pan African Humanitarian & Investment Summit Zanzibar 2022” wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuufungua mkutano huo uliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Unguja Wilaya ya Magharibi “B”. (Picha na Ikulu).
Dkt.Mwinyi amesema hayo katika Kongamano la Saba la Ujumuishi, Utu na Uwekezaji (Pan African Humanitarian & Investment Summit) lilofanyika Novemba 8, 2022 katika Hoteli ya Golden Tulip, Airport Zanzibar.
Amesema, uhifadhi wa mazingira ya bahari ni muhimu katika kufanikisha dhana ya matumizi bora ya rasilimali za sekta za Uchumi wa Buluu, unaohusisha Utalii, Viwanda vya rasilimali za baharini, ufugaji wa samaki, Uvuvi, Mafuta na Gesi asilia.
Amesema, ni muhimu katika uhifadhi wa mazingira bahari kufuata miongozo ya Ulimwengu kama vile mwenendo wa sera pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt.Mwinyi amesema,baada ya kuibuka kwa Ugonjwa wa UVIKO-19, Dunia imeelekeza nguvu katika ukuzaji wa shughuli za kiuchumi wa bahari na hivyo kubadili mandhari ya uchumi wa Dunia, ambapo hali hiyo haitokani na msukumo wa washirika wa maendeleo bali kutokana na michango ya mifuko mbali mbali pamoja sekta binafsi.
Akigusia Kauli mbiu ya Kongamano hilo isemayo ‘Mjadala kuhusu uchumi wa Buluu katika Afrika’ amesema inaakisi dhamira ya kutoa msukumo katika kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia sekta ya uchumi wa Buluu barani Afrika ili kuwa uwekezaji endelevu.
Pia amesema, anaunga mkono mpango huo utakaoshirikisha teknolojia, sera, akinamama pamoja na vijana, kwa kuelewa kuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko katika sekta ya uchumi wa Buluu, na kusema mpango huo ni mwelekeo bora katika kuibadili Afrika ili iwe na uchumi imara.
Ametumia fursa hiyo kuwashajihisha washiriki wa Kongamano hilo kutembelea vivutio vya Utaliii viliopo nchini, baada ya kukamilisha mkutano huo.
Naye Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Suleiman Masoud Makame amesema, kongamano hilo pamoja na mambo mengine litajadili na kuangalia fursa, mianya na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uchumi wa Buluu, ambapo pia litajadili namna ya uhifadhi na uendelezaji wake.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi kwa juhudi zake za kuwaunga mkono na kuwazesha wajasiriamali wa Zanzibar ili waweze kutumia fursa ziliomo katika uchumi wa Buluu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi Maalum kutoka Serikali ya Seychelles na Rais mstaafu wa Seyshelles Mhe.Danny Faure, wakati wa ufungfuzi wa mkutano wa “7th Pan African Humanitarian & Investment Summit Zanzibar 2022, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Unguja Wilaya ya Magharibi “B” .
Naye, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Sychelles, Danny Faure amesisistiza umuhimu wa wadau wote ikiwemo wawekezaji, washirka wa maendeleo, vijana, watunga sera, mabenki pamoja na wamiliki wa viwanda vya rasilimali za bahari kuelekeza nguvu katika uhifadhi wa mazingira ya bahari ili kudumisha ubora wake na kufanikisha dhana ya Uchumi wa Buluu.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Pan African Leadership Developement Centre (PALEDEC), MaryVonne Pool amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi kwa kazi kubwa naayofanya katika kuleta ustawi katika sekta ya uchumi wa Buluu, huku akibainisha kuwepo imara sambamba na kuahidi kutoa nafasi za mafunzo nchini Sychelles kwa vijana watatu wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum ya mfano wa samaki na Balozi wa Heshima wa Seychelles nchini Tanzania, Mhe.MaryVonne Pool, baada ya kuufungua wa mkutano wa “7TH Pan African Humanitarian &Investment Summit Zanzibar 2022”, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Unguja Wilaya ya Magharibi “B”.(Picha na Ikulu).
Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga amesema, kongamano hilo lina azma ya kuwaleta pamoja wadau, ikiwemo wawekezaji na wafanyabiashara ili kujadili fursa za uwekezaji katika uchumi wa Buluu.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta hiyo ambapo zaidi ya kampuni 250 tayari zimewekeza miradi yao, huku Serikali ikiendelea na juhudi za kuimarisha miundo mbinu ya barabara pamoja na bandari kwa lengo la kukuza uchumi wake.
Kongamano hilo pia limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariamu Mwinyi, Mabalozi, Wawekezaji, wafanyabaishara na wajasiriamali.