NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema madhumuni ya binadamu kuletwa duniani ni kumuabudu Mwenyezi Mungu, hivyo amesisistiza wajibu wa waislamu kujifunza dini yao pamoja na kuwafunza watoto wao.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesema hayo Novemba 18, 2022 katika Ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa ‘Masjid Hussein’ ulioko Ghana Kichakani, Wilaya Kati Unguja, hafla iliokwenda sambamba na Ibada ya sala ya Ijumaa.
Amesema, dhamira ya binadamu kuletwa duniani, ni kumcha Mola wake pamoja na kuwafunza watoto elimu ya dini ili waweze kutekeleza dini yao kwa usahihi kama ilivyoamrishwa.
Alhaj Mwinyi ameahidi kuchangia ujenzi wa Madrsa katika eneo la pembezoni mwa msikiti huo pamoja na kufanikisha ujenzi wa uzio kuzunguka msikiti huo.
Amewashukuru waumini na viongozi wao kwa hatua yao ya kuita msikiti huo jina lenye mnasaba na jina lake la ‘Hussein ‘ .
Alhaj Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi, wanakijiji pamoja na waislamu wote waliochangia kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.
Naye, Mufti Mku wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab alisema ana imani kubwa kuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi atafanikiwa kuwaunganisha Wazanzibar kama alivyofanikiwa Mtume Muhammad (SAW).
Aidha, kwa niaba ya wanakijiji wa Ghana Kichakani, Comodo Azana Hassan Msingiri aliishukuru Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja pamoja na ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kati Unguja kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.
Mapema, Katibu katika sala hiyo ya Ijumaa, Ustadhi Rajab Abdillah Haji alitoa ahadi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinfduzi la kuutunza msikiti huo, sambamba na kuutumia kikmailifu kwa ajili ya kutoa elimu ya dini kwa waumini wa maeneo hayo.