RAIS MWINYI AMESHAFANYA MAKUBWA:Yale anawafanyia, nenda ukaangalie

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametimiza miaka miwili ya kuwepo madarakani.

Miongoni mwa mambo ambayo ameyafanya na kuleta matokeo chanya kwa haraka ni kuimarisha demokrasia, umoja wa kitaifa, mageuzi ya sekta ya fedha, biashara, kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kuanzia elimu, afya, miundombinu na kupaisha uchumi.

Ni mafanikio ambayo yamepatikana, licha ya kuingia madarakani katika kipindi kigumu ambacho Dunia ilikuwa inakabiliana na changamoto za UVIKO-19 na madhara hasi yatokanayo na vita vya Urusi na Ukraine.

Aidha, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi akizungumza na wananchi Chake Chake, Pemba kuhusu miaka miwili ya uongozi wake hivi karibuni alisema sekta hizo zimefanikiwa na kueleza kutakuwepo na mafanikio makubwa ya kiuchumi kutokana na watendaji aliowapa dhamana kuwa na ubunifu katika biashara.

Pia ndani ya miaka miwili ya uongozi wake, alisema mafanikio makubwa yamepatikana katika kujenga misingi mizuri ya demokrasia, utawala bora, mikakati ya kifedha na ukusanyaji mapato huku akiwapa majukumu watendaji katika sekta hiyo ambao wapo nje ya mfumo wa serikali yaani sekta binafsi.

“Nilipoingia madarakani nilikuwa na mikakati ya kuziimarisha sekta za fedha ikiwemo mabenki na mashirika ya bima kuona yanafanya shughuli zake na kwenda na kasi ya mageuzi yaliopo sasa na ndiyo maana nikawateua baadhi ya watendaji kutoka sekta binafsi kutoka nje ya Zanzibar kushika nafasi za uongozi,”alisema Rais Dkt.Mwinyi.

Mbali na hayo Rais Dkt.Mwinyi amekua mkali kuhusu wafanyakazi au watumishi wazembe na wabadhirifu wa mali za umma ambapo mara kwa mara amekuwa akichukua hatua za haraka ili kuyaendea maono yake ya kujenga Zanzibar mpya, shirikishi na iliyojaa neema tupu na kuipa sura mpya ya kimaendeleo.

Serikali yake imefungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa ajili ya kushiriki kutekeleza miradi mbalimbali kuanzia uchumi wa buluu na kwingineko ili kufungua fursa za ajira na kustawisha uchumi. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, hii miaka miwili Rais Dkt.Mwinyi kafanya mambo makubwa, endelea;


1.Wenyewe wamsifia, vipi siye tutulie,
Yale anawafanyia, nenda ukaangalie,
Pale walipoanzia, pazuri wapafikie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

2.Kwanza demokrasia, hilo na tuwasifie,
Kuko shwari nakwambia, figisu siangalie,
Serikali kisikia, ni Amani isalie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

3.SUK hiyo angalia, watu iwatumikie,
Wapinzani meingia, sitake tukutajie,
Yale wanaangalia, pazuri wapafikie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

4.Rais tunapitia, ya kwake tuangalie,
Pale lipoikutia, Serikali isalie,
Hilo halikuvutia, kufanya afikirie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

5.Amani tunasifia acha waifurahie,
Na hata machinga pia, yao ayaangalie,
Waweze kujipatia, riziki wafurahie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

6.Kilimo cha mwani pia, vifaa awapatie,
Waweza kujiuzia, bei wazifurahie,
Pazuri wamefikia, mbele wakuangalie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

7.Uchumi buluu pia, na huo tuangalie,
Fursa kufungulia, wenye fedha waingie,
Mali kutuzalishia, kodi nayo iingie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

8.Viwanda vikiingia, ajira tujipatie,
Uchumi utatulia, ulipo usisalie,
Pazuri tutafikia, na sote tufarihie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

9.Wale atuteulia, kazi wamsaidie,
Vema atuchanganyia, vijana awatumie,
Jambo la kufurahia, kuongoza waingie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

10.Wazembe memsikia, hawataki wasalie,
Kwa kweli awafagia, kazini wasibakie,
Na wabadhilifu pia, kortini waingie,
Hii miaka miwili, Mwinyi kafanya makubwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news