NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewatunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi 724 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 03/19 wa Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na kundi la 69/21 Refu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Wanafunzi mara baada ya Kuwatunuku Kamisheni kwa Cheo cha Luteni Usu kwenye Sherehe zilizofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli mkoani Arusha leo Novemba 26, 2022.(Picha na Ikulu).
Akitoa maelezo katika sherehe zilizofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Jeshi (TMA) Monduli, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) Brig. Jen. Jackson Mwaseba amesema kati ya wanafunzi waliohitimu wanawake ni 89 na wanaume 635.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete amesema JWTZ imekuwa ikishirikiana na Chuo hicho kutoa Shahada ya Sayansi ya Kijeshi ambapo kwa kipindi cha miaka 3 ya ushirikiano jumla ya wanafunzi 313 wamehitimu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride la Heshima kabla ya Kuwatunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi 724(Wanaume 635) (Wanawake 89) kwa Cheo cha Luteni Usu katika Sherehe zilizofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli mkoani Arusha.
Aidha, Dkt. Mwaitete amesema Shahada hiyo inawaandaa maafisa waliohitimu kuweza kuwa mahiri katika kusimamia masuala ya kijeshi, amani pamoja na uongozi kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Dkt. Mwaitete pia amesema Chuo cha Uhasibu kina mpango wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa Shahada mbalimbali zikiwemo usalama wa mitandao, usalama na masomo ya kimkakati, masomo ya ulinzi na amani pamoja na ulinzi wa taarifa. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama kwa ajili Wimbo wa Taifa na Ule wa Afrika Mashariki kabla ya Kutunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi 724(Wanaume 635) (Wanawake 89) kwa Cheo cha Luteni Usu katika Sherehe zilizofanyika kwenye Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli mkoani Arusha.
Hali kadhalika, Dkt. Mwaitete amesema Chuo cha Uhasibu kinaunga mkono mpango wa Serikali kupeleka Vyuo vya Elimu ya Juu katika mikoa ya pembezoni kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwatunuku Shahada ya Sayansi ya Kijeshi Wahitimu 109 kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) kwenye Sherehe zilizofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha tarehe 26 Novemba, 2022. Viongozi mbalimbali, Wakuu wa Majeshi Wastaafu, Maafisa wa Juu kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa kwenye Sherehe za Kamisheni kwenye Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli mkoani Arusha.
Pamoja na kutunuku Kamisheni, Mhe. Rais Samia ametoa zawadi kwa Maafisa wanafunzi waliofanya vizuri katika mafunzo hayo.