NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka watunza kumbukumbu na nyaraka za umma kuzingatia weledi wa kazi yao kwa kuhakikisha wanatunza siri za Serikali kwa maslahi ya Taifa.

Rais Samia amesema hayo leo Novemba 27, 2022 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 10 wa Chama cha Taaluma na Menejimenti ya utunzaji Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania uliofanyika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.
Pia Mheshimiwa Rais Samia ameonesha kutofurahishwa na kuvuja kwa taarifa nyeti za Serikali kwenye mitandao ya kijamii ambapo amewaelekeza wanataaluma kuangalia kwa jicho la tatu suala hilo.
Kuhusu suala la matukio ya kupotea kwa nyaraka na taarifa,Rais Samia ametoa wito kwa watunza kumbukumbu hao kuongeza umakini katika usimamizi na uhifadhi thabiti wa nyaraka hizo kwa kuwa kosa moja linaloweza kufanywa na mtunza kumbukumbu linaweza kugharimu maisha ya wengi.

Pamoja na hayo Rais Samia amesema, Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watunza kumbukumbu ikiwa ni pamoja na kupanda kwa madaraja.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amewapatia eneo Chama cha Watunza Kumbukumbu na Nyaraka kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Maarifa.