NA MWANDISHI WETU
TIMU ya Uendeshaji wa Huduma za Afya (RHMT) Mkoa wa Kilimanjaro imeshauriwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wanaofuata huduma katika hospitali za halmashauri na mkoa,huduma ambazo zinapatikana katika zahanati na vituo vya afya

"Asilimia 85 ya wananchi wanatibiwa katika vituo vya afya, kwahiyo tunatakiwa kutoa huduma nzuri katika vituo hivi ili kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa katika Hospitali za Halmashauri na Mikoa ambao wengi wao wanapelekwa wakiwa katika hali mbaya,"ameeleza Dkt.Kapologwe.
Sambamba na hilo Dkt. Kapologwe ameishauri RHMT Kilimanjaro kuendelea kutoa elimu ya afya kwa jamii hususani elimu juu ya magonjwa ya mlipuko ili kuwawezesha wananchi kujikinga na magonjwa ya mlipuko na hatua za kuchukua endapo mwananchi akigundulika kuwa na dalili za ugonjwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt.Jairy Khanga ameishukuru timu ya usimamizi shirikishi kutoka OR-TAMISEMI kwa kufanya ziara katika Mkoa wa Kilimanjaro akisisitiza kuwa ziara hiyo italeta matokeo chanya katika utekelezaji wa shughuli za afya katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Timu ya Wataalam kutoka Idara ya huduma za Afya OR-TAMISEMI ipo mkoani Kilimanajaro kwa ajili ya kufanya ziara ya usimamizi shirikishi katika utekelezaji wa shughuli za afya yenye lengo la kukagua na kushauri namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma za afya katika mkoa huo.