NA ELEUTERI MANGI,WUSM
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahakikishia wa wasanii kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono wasanii wote na kuzitaka sekta za Utamaduni, Sanaa na michezo ziendelee kuwanufaisha vijana wengi zaidi hapa nchini.
Kikundi cha Sanaa cha Taifa Zanzibar wakitumbuiza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Novemba 11, 2022 Bagamoyo mkoani Pwani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akipiga ngoma kuashiria Ufunguzi Rasmi wa Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo Novemba 11, 2022. Tamasha hilo linafanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani.
Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo Novemba 11, 2022 wakati akizindua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani.
“Sanaa ndiyo roho ya taifa lolote pia hatuna budi kuhakikisha tuna Sanaa yenye asili na maadili yanayotuwakilisha sisi Watanzania, nawasihi Watanzania wenzangu na hasa wasanii wetu wa kizazi kipya kuepuka tabia ya kuiga kila tamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili yetu,” amesema Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea zawadi ya picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan iliyochorwa na wanafunzi wa TaSUBa kabla ya kufungua rasmi Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo Novemba 11, 2022 ambalo linafanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani.
Na kusisitiza kuwa “Pale inapolazimika kuiga Sanaa na tamaduni za mataifa mengine, basi mhakikishe mnaiga Sanaa zinazoendana na maadili ya na tamaduni zetu, tusipoteze asili, heshima na utambulisho wetu.”
Makamu wa Rais ameongeza kuwa wasanii wanaweza kuiga yale mazuri yanayofaa na yanaendana na maadili ya Watanzania lakini yale yasiyotufaa tuwaachie wenyewe wenye tamaduni zao na ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kutengeneza maudhui ya kazi zenu na wakumbuke kwa wasanii ni kioo cha jamii, wakitengezeza kazi mbaya jamii haitaheshimu kazi zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka wasanii kutengeneza taswira nzuri katika jamii, walezi na wazazi ambayo haitawafanya wawe wagumu kuruhusu vijana wao kujihusisha na Sanaa kupitia muziki na filamu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea zawadi ya picha yake iliyochorwa na wanafunzi wa TaSUBa kabla ya kufungua rasmi Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo Novemba 11, 2022 ambalo linafanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani.
Aidha, Makamu wa Rais Dkt. Mpango ametoa maagizo nane kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kuendelea kusimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo kikamilifu ili ziendelee kuwa na mchango thabiti katika uchumi wa taifa, kuendelea kusimamia shughuli za michezo na Sanaa vema kuanzia shuleni kwa sababu sasa zinatambuliwa kama taaluma kamili na ajira, viongozi katika mamlaka zote za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waendelee kushirikiana na Wizara yenye dhamana katika kuendeleza shughuli za Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizi.
Maagizo mengine ni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo waendelee kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhifadhi, kutunza na kutangaza tamaduni za makabila yote ya Tanzania kupitia utalii wa kiutamaduni na kutoa nafasi kwa makabila yetu hapa nchini kuonesha tamaduni zake za chakula, dawa za asili, mavazi, makazi na aina za ngoma na burudani zake na kuongeza kuwa kila mkoa uweka utaratibu wake wa kuendeleza utamaduni wa wa mkoa husika iwe sehemu ya utalii wa kiutamaduni wa mkoa huo.
Jambo lingine alilosisitiza Makamu wa Rais ni kutekeleza agizo la Mhe. Rais alilolitoa wakati alipowaita Ikulu timu ya taifa ya Serengeti Girls Julai 2022 kwamba Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Fedha na Mipango ziendelee kujadiliana juu ya namna bora ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Utamaduni ili shughuli muhimu zitakazochagiza ukuaji wa uchumi na ajira kwa vijana kupitia sekta hizi za burudani zisikwame.
“Katika suala hili Mhe. Waziri nataka ripoti au taarifa suala hili limefikia wapi kiutekelezaji wake na naomba taarifa hii inifikie kabla ya Desemba 30, 2022 kabla ya kufunga nusu mwaka ya mwaka wa fedha,” amesema Makamu wa Rais Dkt. Mpango.
Pia ameiagiza wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo washirikiane na wadau husika kuendelea kutoa elimu na kutafuta namna bora ya kutatua changamoto zote zinazohusiana na Hakimili, Hakishiriki, mirabaha na mikataba katika sekta za Utamaduni na Sanaa kwa ujumla wake.
Ameongeza kuwa,Tamasha la Bagamoyo liendelee kuborehwa kila mwaka ili lifikie hadhi ya matamasha mengine makubwa duniani, wizara itoe kipaumbele katika kukitangaza Kiswahili duniani, kuanzisha kituo cha Sanaa cha watoto na vijana wenye vipaji na ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa elimu, kuanza ujenzi wa nyumba changamani na uzalishaji wa filamu, kuanzisha shule maalumu ya kukuza vipaji vya wanamichezo (sports Academy) wazo hili litekelezwe.
Mwisho Makamu wa Rais amesema kuwa tamasha la Bagamoyo liendelee kuzingatia masuala ya Muungano kwa kuhakikisha vikundi vingine zaidi kutoka Zanzibar na sehemu zote za Tanzania Bara vipate nafasi katika tamasha hili. Kwa kutekeleza maagizo hayo, wizara itapiga hatua kubwa sana na kubidhaisha Sanaa na Utamaduni wa mtanzania pamoja na kukuza sekta ya michezo nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kazi ya Wizara hiyo ni kuwaletea furaha na faraja kwa Watanzania pamoja na kubuni mambo mbalimbali ambayo yataleta furaha na Amani katika nchi yetu.
Aidha, Waziri Mchengerwa amesema kuwa tamasha la Bangamoyo limeendelea kuboreshwa na kuwa tamasha la kimataifa ambalo litakuwa na washiriki wengi kutoka nje ya nchi ambapo mwaka huu vipo vikundi kutoka Canada, Zambia, Burundi na Visiwa vya Mayote kutoka nchini Ufaransa.
“Malengo yetu katika tamasha hili na lile la Sauti za Busara kutuka Zanzibar ni kuyaendeleza matamasha haya ili kuyafanya kuwa ya kimataifa, tumeshapokea maelekezo kutoka kwa Mhe. Rais ili kushirikiana nao pamoja kuhakikisha tamasha la Bagamoyo pamoja na Tamasha la Sauti za Busara la Zanzibar yataendelezwa kuwa na taswira ya kimataifa katika siku za usoni hatua itakayosaidia kulitangaza taifa letu ndani na nje ya nchi kimataifa,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa pia amemweleza Mkamu wa Rais kwa Wizara hiyo imeanza kutelekeza program ya mtaa kwa mtaa nchi nzima ili kusaka vijana wenye vipaji katika sekta ya Sanaa na Michezo ili kuvikuza na kuviendeleza na kuwa taifa la watu wenye furaha na Amani kupitia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.