Serikali yaagiza vishikwambi viwafikie walengwa

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imezindua zoezi la ugawaji vishikwambi kwa walimu nchini na kuzitaka mamlaka zinazohusika na kazi hiyo kuhakikisha vishikwambi hivyo vinawafikia walengwa ili viweze kufanya kazi iliyokusudiwa.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema vishikwambi hivyo vinalenga kuboresha mchakato wa utoaji elimu ili kuinua ubora wa elimu nchini, hivyo ni vizuri vikawafikia walengwa ili lengo liweze kutimia.
“Hapa ningependa kusisitiza kuwa vishikwambi hivi ni kwa ajili ya walimu tu na si vinginevyo hivyo Viongozi wote wa Serikali mliopo OR- TAMISEMI, Halmashauri na wale wote watakaokuwa na jukumu la kugawa vishikwambi hivi hakikisheni hakuna mwalimu atakayekosa,” amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita tangu kuingia madarakani imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye TEHAMA ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 - 2025 ambayo inasisitiza matumizi ya TEHAMA katika ngazi mbalimbali za Elimu ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya watu kwa ujumla.
“Walimu hakikisheni mnatumia vishikwambi hivi katika kuboresha mchakato wa utoaji elimu ili kuinua ubora wa elimu nchini na si vinginevyo na naamini mtahamasika katika kutumia TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji,” ameongeza Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara ya Elimu imenunua jumla ya Vishikwambi 300,000 kwa lengo la kuendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji nchini.Amesema vishikwambi hivyo vinakwenda kurahisisha upatikanaji wa nyenzo za kufundishia na kujifunzia, kuongeza idadi ya walimu watakaotumia mfumo wa kujifunzia wa Taasisi ya Elimu Tanzania unaojulikana kwa jina la Learning Management System (LMS) na kuhama kutoka mfumo wa usahihishaji wa mitihani wa makaratasi kwenda mfumo wa usahihishaji wa mitihani kwa njia ya mtandao - (e-marking system).
Mhe. Mkenda ametaja wanufaika wa vishikwambi hivyo na idadi zao kuwa ni Walimu wa shule za msingi za umma ambao watapatiwa 185,404, Walimu wa shule za Sekondari za umma 89,805; Wathibiti Ubora wa Shule ngazi ya Wilaya na Kanda 1,666, Wakufunzi wa vyuo vya Ualimu vya Umma 1,353 na Wakufunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) 297.
Wengine ni Maafisa Elimu ngazi ya Mkoa, Wilaya na Kata ambao watapatiwa vishikwambi 5,772, Wakufunzi wa vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA 996, na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ambao watapatiwa vishikwambi 8,357.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news