Serikali yadhamiria kutokomeza maambukizi mapya ya VVU nchini, wadau wafunguka

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imedhamiria kutokomeza maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuweka mikakati madhubuti ili kufikia malengo hayo ifikapo 2030.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa mwaka wa vijana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe katika ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi tarehe 25 Novemba, 2022 katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Dunia Desemba 1, 2022 wakifuatilia mkutano huo.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu, Bw. Kaspar Mmuya wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa vijana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe na wanawake vijana katika ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi tarehe 25 Novemba, 2022 katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani Desemba 1, 2022.

Kongamano hilo la siku mbili limebebwa na kaulimbiu inayosema; “Imarisha Usawa, Kujilinda ni ibada”
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya akihutubia wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa vijana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe katika ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi tarehe 25 Novemba, 2022 katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Dunia Desemba 1, 2022.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa, katika kuyafikia malengo ni lazima kuwe na mikakati madhubutu inayotekelezeka ili kuhakikisha changamoto ya maambukizi mapya inakwisha nchini ifikapo 2030.

“Ifikapo mwaka 2030 tunapaswa kutokuwa na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI na kuhakikisha hakuna atakayepoteza uhai kwa ugonjwa huo pamoja na kutokomeza unyanyapaa pamoja na jitihada zingine tunaendelea kuwa na mikakakati mbalimbali ya kuweza kutambua afya za watu kwani ni zaidi ya watu milioni moja na laki saba wanaoishi na maambukizi ya UKIMWI,”alisisitiza Mmuya.

Aidha alisema kuwa serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU zinaendelea kupatikana kwa wingi na kwa wakati ili kila mmoja aendelee kuwa na afya njema na kulitumikia taifa letu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Dkt. Leonard Maboko akizungumza wakati wa kongamano hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini,Dkt. Leonard Maboko akieleza mikakati ya Tume hiyo katika kupambana na maambukizi mapya alisema, kundi kubwa linaloongoza katika maambukizi mapya ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 nchini.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana wanaoishi na VVU,Bi Pudenciana Mbwiliza akizungumza wakati wa mkutano huo.

Dkt. Maboko alisema, miongoni mwa sababu zinazochangia kundi la vijana kuongoza katika maambukizi mapya ni pamoja na; vijana kuendeleza mapenzi katika umri mdogo, kukosa malezi mazuri, kuendekeza mihemko na kuwa na mahusiano na watu wenye umri mkubwa pamoja na hali duni ya uchumi.

“Tabia ya kuendekeza ngono maarufu kama kupiga shoo na kupenda masponsor, hii inakwamisha jitihada za Serikali katika mapambano haya kwani vijana wameendelea kuishi na kufuata tabia hizo na kusahau tabia njema ya kumcha Mungu inazowasaidia wengi katika kushinda tamaa za ujana,”alisema Dkt. Maboko
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa mwaka wa vijana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe katika ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi tarehe 25 Novemba, 2022 katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Dunia Desemba 1, 2022 wakifuatilia mkutano huo.

Aliongeza kuwa, pamoja na takwimu hizo bado Serikali haijaacha kuwa na mikakati mbalimbali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kutoa fursa kwa vijana kuondokana na changamoto zao ikiwemo za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Mwitikio wa Kitaifa TACAIDS Bi. Audrey Njerekela akitoa utambulisho wakati wa mkutano huo.

“Kongamano hili limehusisha vijana na viongozi wa dini kwa kuzingatia mchango wao katika kuendelea kusaidia mapambano haya ikiwa ni pamoja na kukemea matukio ya unyanyapaa na kuhimiza matumizi ya ARV kwa wanaogundulika kuwa na maambukizi huku wakihimiza vijana kuendelea kumcha Mungu na kujitenga na uovu,"alisisitiza Dkt.Maboko.

Awali, akitoa salamu zake Sheikh Hilary Shewaji maarufu kwa jina la Kipozeo alipongeza jitihada za Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwashirikisha katika kongamano hilo kwa kuzingatia mchango wanaoutoa katika masuala ya kiimani kwa jamii zetu.
Alisema, ukosefu wa mafundisho ya imani yamechangia mmomonyoko wa maadili inayochochea vijana kujiingiza katika makundi hatarishi yanayochochea ongezeko la maambukizi mapya kwao.

“Vijana wakubali kujifunza elimu ya kimungu ili kuondokana na changamoto za maadili mabaya kwa kuzingatia zipo tamaduni potofu ambazo lazima tuzipinge na kujilinda kuwa salama,” alieleza Sheikh Kipozeo.Naye Mchungaji Mstaafu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Ushirika wa Kigogo KKKT, Richard Hananja maarufu kwa jina la Rich Bilionea alieleza mikakati ya kanisa katika kuwafikia vijana na kueleza kuwa ukosefu wa maarifa unaleta matokeo hasi kwa kundi la vijana wanaotegemewa na kanisa, familia na Taifa kwa ujumla na kuwaasa kuwepo na jitihada za makusudi juu ya elimu ya kiroho ili kusaidie vijana kulindwa na Mungu.

Mchungaji Hananja alisema elimu ikiwepo kwa uwazi italeta mabadiliko ya kimtazamo kwa vijana katika mapambano ya masuala ya UKIMWI ili kusaidia kundi hili.

“Vijana asiwepo mtu anayeudharau ujana wako, kuwa mwenye kupenda maarifa ili kujilinda usiingie katika matendo maovu yanayopelekea kuambukizwa magonjwa, kipekee niwaase vijana kuchakalika kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi inayowasababisha kukimbilia hao masponsor,”alisisistiza mchungaji Hananja.
Naye Mwakililishi wa Baraza la Maaskofu kanisa la K.K.K.T Lindi Mch Dkt. Wayzimen Simwinga alieleza kuwa, vijana hawana budi kupambana katika maisha kuhakikisha wanajilinda na kulinda wengine.

“Maisha ni mapambano, hivyo kujua si kutenda hakikisha unajua vitu na kuvitendea kazi kwa umakini, mnazijua amri za Mungu ila hamzitendei kazi, wito mkubwa kila mtu ajue Mungu yupo, na msidhubutu kuwa mbali na Mungu maana ndiye atupaye mambo yote,” alisiitiza Dkt. Simwinga.

Aidha aliwaasa vijana kuendelea kufanya mema ikiwemo kukataa dhambi ya zinaa inayochangia ongezeko la maambukizi mapya ya VVU kwa vijana kwa kujiingiza katika makundi maovu, hivyo bado msaada ya Mungu unahitajika.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa mwaka wa vijana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe katika ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi tarehe 25 Novemba, 2022 katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Dunia Desemba 1, 2022 wakifuatilia mkutano huo.

“Vijana wengi mnapuuza masuala ya Mungu hii haifaii, mjichunge, mjipende na mjithamini msimuache Mungu, mjali mambo ya Mungu ili atulinde na kutuponya”alisisitiza Dkt. Simwinga.

Alisisitiza kuwa, kila kijana awe kinara katika eneo la upimaji na kujua hali yake na kutumia dawa wanapotambulika na maambukizi huku akiwasihii kuondoa hofu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news