Shafiq Batambuze wa Singida Big Stars ashikwa 'uchawi' wakicheza na Simba SC

NA DIRAMAKINI

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imemfungia mechi tatu na faini ya shilingi laki tano mlinzi wa kushoto wa Singida Big Stars, Mganda Shafiq Batambuze.

Ni kwa kosa la kuingia uwanjani kuanza kupasha moto misuli dakika 10 kabla ya muda ulioainishwa kwenye ratiba ya matukio ya mchezo kuelekea mchezo dhidi ya Simba SC uliomalizika kwa sare ya 1-1.

Mchezaji huyo alipinga maelekezo ya Mratibu wa Mchezo (GC) na Kamishna wa Mchezo waliomtaka arejee chumbani hadi muda uliopangwa utakapowadia.

Akiwa uwanjani, Shafiq Batambuze alionekana kumwaga vitu kwenye majani jambo lililoashiria imani za kishirikina.

Pia Kamati imewafungia michezo mitatu na kuwatoza faini ya shilingi milioni moja kila mmoja, Kocha Msaidizi wa Singida Big Stars, Mathias Lule na Kocha wa Makipa wa timu hiyo, Steven Kiagundu kwa kosa la kumuamuru Shafiq Batambuze aendelee kusalia uwanjani hata pale mchezaji huyo alipojaribu kuondoka.

Timu ya Singida Big Stars imetozwa faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la kushindwa kuhudhuria mkutano wa wanahabari uliopangwa kufanyika Novemba 8, 2022 kwenye ukumbi wa Benki ya NBC tawi la Singida, kuelekea mchezo tajwa hapo juu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news