NA MWANDISHI WETU
KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula amesema, kilichofanikisha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Determine Girls ni kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia baada ya kucheza kwa presha kipindi cha kwanza.
Mtanange huo wa Kundi A, ulipigwa Novemba 2, 2022 katika dimba la Stade Moulay Hassan (Stade Prince Héritier Moulay El Hassan) lililopo jijini Rabat nchini Morocco.
Lukula amesema, kipindi cha kwanza walipoteza nafasi nyingi ambazo ziliwafanya kucheza kwa presha na kufanya makosa kadhaa.
Ameongeza kuwa, baada ya kwenda mapumziko alizungumza na wachezaji na kuwaambia watulie na kucheza kawaida na hicho ndicho kilichosababisha wapate ushindi.
“Ni furaha kwangu kupata ushindi wa kwanza kwenye michuano mikubwa hii, tulicheza vizuri, lakini tulipoteza nafasi nyingi kipindi cha kwanza na kutufanya kucheza kwa presha,”amesema Lukula.
Opa Clement alitupatia bao la kwanza dakika ya 53 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Olaiya muda mfupi baada ya kuingia.
Kocha Lukula aliwaingiza pia Dotto Evarist na Philomena Abakah kuchukua nafasi za Silvia Mwacha na Asha Djafar ambao nao waliifanya timu kuwa imara zaidi.
Olaiya aliwapatia bao la pili kwa mkwaju wa penati dakika ya 79 baada ya Joelle Bukuru kufanyiwa madhambi ndani ya 18.
Nahodha wa Determine Margaret Stewart alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa ya pili ya njano baada ya kumchezea rafu Opa dakika ya 88.
Mchezo wa Simba Queens wa mwisho wa hatua ya makundi utakuwa Jumamosi Novemba 5 dhidi ya Green Buffaloes kutoka Zambia.