NA PETER STEPHEN
MABINGWA Watetezi wa Ligi ya Netiboli ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, timu ya Tamisemi Queens kutoka Dodoma, kwa mwaka wa pili mfululizo imefanikiwa kulitetea kombe hilo baada ya kuibwaga timu ya KVZ kutoka Zanzibar kwa magoli 56-40 katika mchezo mkali na wa kusisimua uliochezwa leo katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali watu (aliyevaa suti ya michezo nyekundu) wa Ofisi ya Rais Tamisemi Bw. Victor Kategere akilinyanyua kombe la ligi ya muungano ya Netiboli baada ya timu yake kuifunga KVZ magoli 56-40.
Tamisemi Queens ambayo inajivunia kuwa na wachezaji watano wanaounda timu ya Taifa ya netiboli waliuanza mchezo huo kwa pasi zao za haraka haraka walifanikiwa kuongoza katika vipindi vyote vya mchezo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni na Michezo, Mhe. Pauline Gekul.
Hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika Tamisemi Queens walikuwa mbele kwa magoli 12-11, na katika robo ya pili wachezaji wa Tamisemi wakiongozwa na Mchezaji bora wa mashindano hayo Mersiana Samwel walimaliza wakiwa na magoli 26-20, huku hadi robo ya tatu ya mchezo inakamilika Tamisemi walikuwa mbele kwa magoli 37-28.
Wachezaji wa KVZ licha ya kuonyesha upinzani mkali katika kipindi cha kwanza, hawakuweza kukimbizana na kasi ya wachezaji wa Tamisemi Queens waliokuwa wakiongozwa na ‘MVP Mersiana Samwel, na Mfungaji bora wa mashindano hayo Lilian Jovin.
Wachezaji wa Tamisemi Queens wakicheza mbele ya Mkurugenzi wao wa Utawala na Raslimali Watu Victor Kategere walidhamiria kulichukua kombe hilo kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kucheza kwa ustadi kiasi cha wachezaji wa KVZ kushindwa kwenda na kasi ya mchezo huo.
Nahodha wa Tamisemi Queens Dafrosa Luhwago akipokea kombe la ubingwa wa ligi ya muungano ya Netiboli iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kufuatia kukamilika kwa mashindano hayo, Timu nne za kutoka Tanzania Bara na Timu nne kutoka Zanzibar zimechaguliwa kushiriki mashindano ya ligi ya netiboli kwa nchi za Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Rose Mkisi amezitaja timu hizo kuwa ni Tamisemi, JKT Mbweni, Nyika na Magereza Tanzania na Zanzibar itawakilishwa na KVZ, Mafunzo, JKU na Zimamoto.