TIANANMEN SQUARE BEIJING: Bendera zikipepea, ziara ya Rais Samia kuanza leo hadi Novemba 4

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya Kitaifa nchini China kuanzia leo Novemba 2 hadi Novemba 4, 2022 kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping.

Bendera za Tanzania na China zikipepea katika eneo Tiananmen Square jijini Beijing kwa ajili ya ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini China inayoanza leo Novemba 2, 2022. (Picha na Ubalozi wa Tanzania-Beijing).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, ziara hiyo ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa juu kutoka bara la Afrika tangu Rais Xi Jinping achaguliwe tena na Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kwa muhula wa tatu.

Vilevile, ziara hiyo itakuwa miongoni mwa ziara za mwanzo za viongozi wa kitaifa kutembelea nchini China tangu utokee mlipuko wa UVIKO-19 mwezi Desemba 2019.

Rais Samia atapokelewa rasmi tarehe 3 katika ukumbi wa Great Hall of the People ambapo atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais wa China, Xi Jinping na kushuhudia utiaji saini wa mikataba mbalimbali.

Mbali na kukutana na Xi Xinping, Rais Samia anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang pamoja na Spika wa Bunge la nchi hiyo Li Zhanshu.

Ziara ya Rais Samia inafanyika katika kipindi ambacho Tanzania na China zimeadhimisha miaka 58 ya mahusiano ya kidiplomasia. Viongozi hao wawili wanatarajia kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za siasa, uchumi, utamaduni na ushirikiano wa kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news