NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi katika hospitali mpya ya Mkoa wa Mjini Magharibi, inayoendelea kujengwa katika eneo la Lumumba.
Akizungumza na viongozi, watendaji na wananchi walioshiriki katika ziara hiyo, Dkt. Mwinyi alisema amefurahishwa na kasi ya Mkandarasi anayeendeleza mradi huo, ambapo hadi sasa hatua za ujenzi zimefikia asilimia 69 ya kazi yote.
Amesema, kuna kila sababu ya kujivunia kwa uwepo wa hospitali hiyo ambayo ni ya aina yake hapa Zanzibar.
Aidha, amebainisha azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha kila mkoa hapa nchini unakuwa na hospitali ya aina hiyo.
Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi amewatoa hofu wajasiriamali wanaojihusisha na kazi za kutengeneza vyombo vya moto ambao wamelazimika kusimamisha shughuli zao na kuhama eneo hilo ili kupisha ujenzi wa hospitali hiyo.
Amewathibitishia wajasiriamali hao kuwa, tathmini kwa ajili ya malipo yao tayari imefanyika na wanatarajiwa kulipwa katika kipindi kifupi kijacho.
Aidha, amewahakikishia kuwekewa miundombinu muhimu katika sehemu yao mpya kazi.