UTHUBUTU WANAWAKE:Kujifungiafungia, sawa na kujilisha sumu

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 28, 2022 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wawe na uthubutu katika siasa na uchumi.

Amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa 10 wa (UWT) ambao pamoja na mambo mengine, ulifanya Uchaguzi Mkuu wa jumuiya hiyo.

“Wanawake wengi wetu tunajifungia, tunauendekeza uanamke hata tukiwa kwenye vikao…ukiwa na mawazo unashindwa kuzungumza unaogopa kukosolewa au kulaumiwa na usiposema unarudisha taasisi nyuma. Ni uthubutu pekee unaweza kuifanya taasisi isonge mbele sio unajua kitu unashindwa kusema unaogopa kulaumiwa unaogopa kunyimwa kura,” alisema Rais Samia.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, moja wapo ya nguvu kubwa ya ya kuzisukuma ndoto na malengo yako ni kuonesha uthubutu, hivyo uthubutu wa wanawake ni muhimu kwa sasa na wakati ujao, endelea;


1:Uthubutu wanawake, uthubutu ni muhimu,
Mkitaka msitake, hapo muwe vichwa ngumu,
Na nyie mueleweke, mshike kazi muhimu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

2:Amesema wanawake, wengi ni wagumugumu,
Kujiendekeza peke, huku mnayo swaumu,
Sasa muda muamke, kazi mshike hatamu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

3:Ni Rais mwanamke, asema hata muhimu,
Kawaona wanawake, mnasuasua humu,
Lengo ataka mtoke, hivyo pokea salamu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

4:Kujifungiafungia, sawa kujilisha sumu,
Na kutozungumzia, yenu muweze jikimu,
Chini chini mwasalia, kati yao wanadamu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

5:Ni uthubutu pekee, utawafanya watamu,
Nafasi mzipokee, zile mnazifahamu,
Maisha yaendelee, juu mtese kwa zamu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

6:Sifa moja wanawake, kwao hii inadumu,
Ifike wachagulike, kazi waingie zamu,
Wafanya watambulike, jinsi walivyo timamu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

7:Uaminifu mkubwa, kwao ni tunu muhimu,
Ni kama kula ubwabwa, rushwa hawazifahamu,
Wanayatenda makubwa, pasipo na udhalimu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

8:Fursa za kiuchumi, kuzishika ni muhimu,
Haijalishi usomi, uthubutu uwe hamu,
Ni maneno ya ulimi, lakini yalo adhimu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

9:Uwezo wa kiuchumi, kwenye maisha muhimu,
Kwenye siasa huzami, unakuwa ni timamu,
Usikae hujitumi, hali itakuwa ngumu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

10:Tuna Rais Samia, kileleni ametimu,
Wanawake angalia, na nyie iwape hamu,
Kwa siasa kuingia, hata ziwepo shutumu,
Hebu vamia siasa, jiongeze kiuchumi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news