NA FRESHA KINASA
KATIKA kutokomeza vitendo vya ukatili wa Kijinsia Shirika lisilo la kiserikali la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma mkoani Mara limeendesha tamasha katika Kata ya Rusoli lililohusisha ngoma za asili, zeze, kwaya, na mchezo wa mpira wa miguu uliozikutanisha timu ya Kata ya Rusoli na Kata ya Msanja wilayani humo kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya mapambano ya vitendo hivyo.

Hatua hiyo, ni sehemu ya majukumu ya mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia maeneo ya mialo unaotekelezwa na Shirika hilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Musoma ambao umeanza kutekelezwa mwezi septemba 2022, hadi Aprili 2023 chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society.

Maingu amewataka pia wanananchi kutambua viashiria vya ukatili wa kijinsia na kuchukua tahadhari mapema kabla ya matukio kutokea, kwani yanapotokea yamekuwa na madhara katika familia na katika jamii ikiwemo kuchangia mmomonyoko wa maadili, ulemavu na kurudisha nyuma maendeleo.

Pia, amewataka wazazi, walezi na jamii kuungana kwa pamoja kusimamia malezi kwa watoto na kuwapa mahitaji yao ya msingi sambamba na kuwajibika kusimamia haki zao katika kuwaandaa kuja kuwa msaada kwa jamii na taifa kwa siku za usoni.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Vincent John amewahimiza wananchi hao kuachana na tabia ya kujichukulia hatua mkononi kinapotokea kitendo cha ukatili kwani kufanya hivyo ni kinyume kwa mujibu wa sheria za nchi.


Mariam Peter mkazi wa Rusoli amesema kuwa, wanaweke wamekuwa wakikumbana na ukatili wa vipigo kutoka kwa waume zao jambo ambalo ni unyanyasaji na ni ukatili usiofaa kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Unakuta mwanaume ameondoka nyumbani anarudi usiku wakati huo hajaacha hata hela ya matumizi mwanamke amepambana na kazi ndogo ndogo amelipwa hela kidogo amenunua chakula watoto wamekula na pia ameacha chakula cha mwanaume. Amekaa amengoja hadi saa nne usiku mwanaume hajarudi anakwenda kulala, mwanaume akija anakuwa amelewa anabisha mlango mwanamke akikawia kufungua mlango tu kidogo anapewa kipigo na matusi huo ni ukatili ambao katika maeneo yetu upo wanaume wanaufanya," amesema Mariam Peter.
Janeth Peter amesema kwamba, wanaume wamekuwa wakifanya maamuzi bila kuwashirikisha wanawake hasa uuzaji wa rasilimali mbalimbali katika familia yakiwemo mazao na mifugo na kutumia fedha zote.
"Mnalima pamoja mazao, mnafuga mifugo katika familia, lakini mwanaume anapotaka kuuza mfugo baadhi yao hawaulizi wake zao au kushirikisha watoto wanauza tu kwa kujiamulia. Mwanamke akiuliza anakumbana na kupigwa au kusimangwa kwamba mali hazimhusu wakati ameshiriki mwanzo mwisho katika uzalishaji huo. Anakaa kwenye ndoa kwa kunyanyasika anaona akiondoka watoto watapata mateso," amesema Janeth Peter.
