NA FRESHA KINASA
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Mheshimiwa Charles Manumbu amelipongeza Shirika la Victoria Farming and Fishing (VIFAFIO) kwa juhudi zake za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia uliozoeleka katika maeneo ya uvuvi.
Mheshimiwa Manumbu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Iramba ameyasema hayo Novemba 12, 2022 wakati akikabidhi zawadi kwa washindi wa Tamasha la Funguka kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia uliozoeleka katika maeneo ya jamii za wavuvi lililofanyika katika Kijiji cha Isanju wilayani Bunda.
Ambapo tamasha hilo limejumuisha washiriki wa ngoma za asili, mpira wa miguu na mpira wa pete kutoka kata za Chitengule na Iramba likilenga kuwaelimisha wananchi na kuwashirikisha katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
"Naendelea kutambua umuhimu wa wadau hasa Shirika la VIFAFIO kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society, naunga mkono juhudi zao kwa kuwakutanisha kwa mara nyingine wachezaji wa mpira wa Miguu kata za Chitengule na Iramba kwa mashindano ambapo mshindi atapewa zawadi ya fedha shilingi 200,000 na kila timu itapatiwa mpira mmoja. Hatua hii ni muhimu na ya kupongeza katika kutokomeza ukatili,"amesema Charles Manumbu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Tamasha hilo lilioandaliwa na VIFAFIO kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society pamoja na kuwepo kwa burudani mbalimbali pia elimu ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia imetolewa na wawezeshaji Neema Milanzi na Maria John ambao ni maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
"Katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo na mamlaka zinazohusika na utoaji wa haki kwa wahanga wa ukatili," amesema Neema Afisa Ustawi Bunda.
Katika tamasha hilo wananchi wameelimishwa juu ya dhana ya ukatili wa kijinsia, aina za ukatili wa kijinsia, visababishi vya ukatili, viashiria vya ukatili, madhara ya ukatili na hatua za kuchukua pindi vitendo vya ukatili vinapofanyika katika jamii.
Kwa upande wake mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Victoria Farming and Fishing, Robinson Wangaso amesema ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka ambalo linapaswa kushughulikia na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wahanga wanapatiwa huduma sahihi ukiwa ni pamoja na matitabu, msaada wa kisheria, ushauri nasaha na huduma nyinginezo.
Wangaso amesema Idara ya Ustawi wa jamii ndiye mratibu mkuu wa wadau katika kutoa huduma sahihi kwa wahanga, hivyo waathirika wahudumiwe kwa ushirikiano baina ya watoa huduma wote.
"Hakuna ukatili mdogo wala mkubwa, madhara au athari za ukatili ni kubwa kuliko jamii inavyofikiri,"amesema Wangaso.
Neema Paul mkazi wa Isanju amelipongeza shirika la VIFAFIO kwa kupeleka elimu hiyo kwa wananchi ambapo amesema, itakuwa chachu ya kuleta mabadiliko kwa wananchi katika kuunga mkono mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili uliozoeleka maeneo ya uvuvi.