NA ANTHONY ISHENGOMA-WANMM
KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amewataka wadaiwa sugu wa kodi ya Pango la Ardhi kulipa kodi hiyo kabla ya Serikali kuanza kuchukua hatua za kisheria kwani wale watakao endelea kukaidi agizo hilo wako hatarini kupoteza milki ya ardhi zao.
Baadhi ya wajumbe wa kikao kazi kati ya Benki ya CRDB na wasimamizi wa kodi wa Wizara ya Ardhi kutoka mikoa yote Nchini wakiwa katika kazi kujadili namna bora ya ushirikaji CRDB katika makusanyo ya pango la kodi ya Ardhi leo Jijini Arusha. (Picha na Hassan Mabuye).
Dkt.Kijazi amesema, suala la kulipa kodi ya ardhi ni la kisheria hivyo kuwataka wananchi wote kuzingatia matakwa ya kisheria kwa kulipa kodi hiyo na kuwakumbusha kuwa Serikali imetoa msamaha wa riba kwa walipa kodi sugu na mwisho wa msamaha huo ni Disemba mwaka huu.
Dkt.Kijazi amesema hayo leo Novemba 4, 2022 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya Benki ya CRDB na wasimamizi wa kodi wa Wizara ya Ardhi kutoka mikoa yote nchini kujadili namna bora ya ushirishaji wa CRDB katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi.
Katibu Mkuu Dkt. Kijazi amesema madeni ya kodi ya Ardhi ni takribani Bil.70 na kusisitiza kuwa hata kama msamaha wa riba ya kodi ya ardhi kukoma Disemba mwaka huu bado wataendelea kudai malimbikizo ya kodi ya ardhi kwa wale watakaoendelea na kumilki ardhi bila kulipa kodi.
Aidha Kiongozi huyo wa Wizara ya Ardhi amesisitiza Taasisi za Umma kuona ya haja ya kulipa kodi ya pango la ardhi kwani kwa sasa malimbikizo hayo yanazihusisha pia taasisi za umma na binafsi na uzoefu unaonesha kiwango kinachokusanywa kidogo kulinganisha na uhalisia kwa idadi ya walipa kodi.
Dkt. Kijazi pamoja na mambo mengine amesisitiza suala la elimu kwa umma kwa wananchi ili kuwajengea uelewa wa masuala ya ulipaji kodi ili waweze kushiriki kikamilifu na kuona umuhimu wa kulipa kodi ya ardhi.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Gerald Kamugisha amesema kimsingi Benki yake iko tayari wakati wowote kufanya kazi na Serikali katika suala la ukusanyaji kodi na tayari kuna matawi kama 50 yanayofanya kazi na Wizara ya Ardhi katika kuhakikisha miamala ya ukusanyaji kodi inafanyika kupitia matawi hayo yaliyoko Dar es Salaam na Pwani.
Kamugisha ameongeza kuwa CRDB imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na imeongweza wigo wa huduma zake hadi nje ya Nchi kwani tayari ina matawi Burundi na inakusudia kufungua matawi yake Nchini Kongo.
Kamishna wa Ardhi Nchini Bw. Mathew Nhonge amesema Wizara ya Ardhi Pamoja na kuwa mtandao mkubwa ukusanyaji kodi ya ardhi mpaka ngazi ya Halmashauri Wizara imeona ni vyema kutumia taasisi na mitandao ya simu ili kupunguza gharama kwa walipa kodi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo katika ofisi za serikali.
Kamishna Nhonge ameongeza kuwa Wizara ya ardhi pia kwa kufanya hivyo inapanua wigo wa wa ukusanyaji kodi ndio maana inaenda mbali zaidi kuboresha mtandao wa ukusanyaji kodi kwa kutumia taasisi za fedha kama Benki na mawakala wa mitandao ya simu Pamoja na Benki.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika juhudi zake za kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi ya Ardhi inajipanga kushirikisha taasisi za kifedha ikiwemo CRDB na baadhi ya makampuni ya simu ili kurahisisha wigo wa ukusanyaji kodi ya pango la Ardhi nchini.