NA HAPPINESS SHAYO-WMU
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewaasa wadau wa misitu kote nchini washiriki kikamilifu katika usimamizi na utunzaji wa maeneo ya misitu ya vijiji ili kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi.
Ameyasema hayo leo Novemba 15, 2022 wakati wa ufunguzi wa warsha ya 22 ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) mkoani Morogoro.
"Kasimamieni misitu vizuri msigawe maeneo hovyo, mkaweke mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuzuia uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi," Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, amewataka viongozi wa MJUMITA wawaelimishe wananchi juu ya usimamizi wa misitu na umuhimu wa uhifadhi.
Katika hatua nyingine Mhe. Mary Masanja amewataka viongozi hao wakemee mila potofu ambazo zinamkandamiza mwanamke na kumnyima fursa za kushiriki kwenye uhifadhi wa misitu .
'Tuchukue hatua mara moja kuhakikisha jinsia inazingatiwa ili kulinda misitu yetu na kuhakikisha jamii inanufaika na uwepo wa misitu hiyo," ameongeza.

