NA ADELADIUS MAKWEGA
WAKRISTO wameambiwa kuwa wajiandae, wajiweke tayari kwa kuwa sasa wameanza dominika ya kwanza ya majilio wanasubiria ujio wa Yesu Kristo anapozaliwa katika roho zao, awakute wapo tayari kumpokea, akifahamu kuwa anaingia katika nyumba zilizolindwa vizuri na kulindwa huko ni kuonesha upendo kwa ndugu jamaa, familia na marafiki.
Mahubiri hayo yametolewa na Katekista mmojawapo ambaye ni miongoni mwa wanafunzi walifundishwa Ukatekista wa Padri Paul Mapalala katika misa ilivyongozwa na Padri Mapalala Jumapili ya Novemba 27, 2022 katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
“Katika hayo yote tunapozidi kujidharau, kudharau wengine, kuwashusha wenzetu na zaidi kujikweza sisi, mambo hayo tunafananishiwa na kipindi kile cha Nuhu.
"Leo tunaambiwa kuwa tunavyoishi katika jamii zetu, Mungu haonekani katika macho ya nyama kama tunavyojiona sisi lakini jinsi tunavyoonana sisi kwa sisi, tunamuona Mungu, jinsi tunavyotendea sisi kwa sisi, tunamtendea Mungu, hivyo tudumu katika upendo, tudumu katika kuthaminiana, ndiyo maana Yesu anatuambia kama mwenye nyumba angejua ni lini mwizi atakuja, angekesha mwizi asije kuvunja nyumba yake, tuwe tayari.”
Misa hiyo pia iliambatana na maombi sita na mojawapo lilikuwa ni hili,“Uwaongoze viongozi wote kujiandaa kutoa hesabu mbele yako kuhusu utawala wa uongozi wao, Ee Bwana.”
Wakati misa hiyo inasaliwa hali ya hewa ya eneo la Chamwino Ikulu kwa juma zima imeendelea kuwa ya Jua kali, Mawingu na Manyunyu kiasi.