NA DIRAMAKINI
JUMUIYA ya Wakulima Mkoa wa Manyara imesena kamwe hawatasikiliza maneno ya wanasiasa wanaotaka kuwagombanisha wakulima na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maslahi yao binafsi.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twange wakulima hao wamesema wako pamoja na Rais Samia mpaka mwaka 2030 na wataendelea kuwapuuza wanasiasa wanaowashawishi wasitoe pongezi zao kwa Serikali kutokana na mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Samia.
"Tunajua kuna wanasiasa, wanatuonea wivu sisi wakulima kwa sababu ya mambo makubwa tunayofanyiwa na Rais Samia na Serikali yake, sisi tunakupongeza na kukutia moyo usichoke kutufanyia mambo makubwa na tukuhakikishie hatutasikiliza kelele za wanasiasa waliojichokea tuko pamoja na Rais Samia mpaka 2030,"amesema Kiongozi wa Jumuiya ya Wakulima Manyara, Alli Athuman Mwiyombo.