NA JOHN MAPEPELE
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imetekeleza ahadi ya (Royal Tour) kuwapeleka washindi wote wa Mashindano ya Dunia ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa viziwi na viongozi kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha.
Washindi wa shindano hao wameanza ziara ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro leo Novemba 1, 2022.
Mashindano
hayo yamefanyika Oktoba 29, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano
wa Julius Nyerere (JICC) jijini Dar es Salaam ambapo yaliwashirikisha
wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Mhe. Mchengerwa amesema, tayari washindi wapo katika siku ya kwanza ya ziara ya kwa gharama za Serikali.
Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amesema, dhamira ya Serikali kwa sasa ni kutumia michezo, Sanaa na utamaduni kuitangaza Tanzania duniani na kuinua uchumi wake.
"Tunatarajia washindi hawa watafurahia vivutio mbalimbali vilivyopo kwenye Hifadhi ya Ngorongoro na watakuwa mabalozi wazuri watakaporejea katika nchi zao,"amesema.
Katika shindano hilo, mtanzania Hadija Kanyama ametwaa taji la Dunia la Urembo, wakati kwa upande wa Utanashati mtanzania Rajan Ally ameibuka mshindi wa pili na mtanzania mwingine Russo Songoro ameshinda taji la wanaume upande wa mitindo.
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika na ya 12 duniani kuandaa na kuwa mwenyeji wa shindano hilo.