NA MWANDISHI WETU
WAZIRI
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amewataka
watoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kutobadilisha vifurushi
vya vya Inteneti hadi pale watakapotoa bei elekezi Januari 2023.
Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Novemba 21, 2022
kuhusiana na kukamilisha wanabodi ya watumiaji na watoa huduma za
inteneti nchini.
Amesema
wako katika hatua za mwisho kukamilisha tathmini ya gharama za huduma
za mawasiliano nchini na kwamba wanategemea kushusha gharama za
vifurushi hivyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Novemba 21, 2022 jijni Dar es Salaam, Nape
alisema kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala wa vifurushi mbalimbali
vya simu ikiwemo intaneti huku watumiaji wakihoji hatua zinazochukuliwa
na serikali.
Amesema
kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikifanya tathmini kila
baada ya miaka mitano na kwamba tathmini ya mwisho imefanyika mwaka 2018
huku gharama za huduma hizo zikiwa kati ya Sh 2.03 na 9.35.
"Watumiaji
wa huduma wengi wameeleza kuwa hawafurahishwi na huduma za mawasiliano
zinazotolewa na hakuna mawasiliano mazuri kati ya watumiaji na watoa
huduma hivyo kusababisha malalamiko juu ya huduma na hatua
zinazochukuliwa na serikali." Amesema Nape.
"TCRA
inafanya tathmini kila baada miaka mitano na Desemba 2022 itakamilika,
hivyo matokeo yatatolewa Januari kwahiyo nawaomba watoa huduma
kutofanya mabadiliko yoyote ya bei za bundle (Vifurushi)katika kipindi
hiki ambacho tathmini inaendelea hadi itakapokamilika."
Ameongeza
kuwa katika tathmini hiyo inaangalia uwekezaji uliofanywa na kampuni za
simu na kodi wanayolipa ili kuwa na bei elekezi na mategemeo yao ni
kushusha gharama hizo kwa kiasi fulani.
Aidha,
ameongeza siku saba kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano kuomba
nafasi za ujumbe wa bodi ya Baraza la Ushauri la Watumia huduma za
Mawasiliano (TCRA -CCC).
Nape
alisema baraza hilo limekuwepo tangu TCRA ilipoanzishwa lakini
haijulikani hivyo wanalenga kuimarisha baraza hilo ili liwasaidie
kutengeneza mahusiano mazuri kati ya watoa huduma na watumiaji.
Amesema
baraza hilo lina majukumu ya kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma
za mawasiliano, kupokea na kusambaza taarifa za maoni ya wadau, kuwa na
kamati ya watumiaji wa huduma ngazi za mikoa na kufanya mashauriano na
wahusika katika sekta hiyo.
"Baraza
lingekuwa na nguvu lingesimamia mahusiano yaliyopo kati ya watoa huduma
na watumiaji lakini baraza hilo bodi yake imetetereka hivyo tumeongeza
siku za maombi ili kupata wajumbe wa bodi," alisema.
Amesema
jukumu la kwanza la bodi hiyo ni kukusanya maoni ya watumiaji wa huduma
za mawasiliano kuhusu utendaji, kanuni na sheria kisha wazipeleke
kwenye wizara kwa lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano
zinaboreshwa.
Ameeleza
kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha linaondoa malalamiko na
kutoelewana baina ya watumiaji wa huduma na watoa huduma za mawasiliano
nchini.