WATORO WA IMANI

NA ADELADIUS MAKWEGA

MSOMAJI wangu katika matini iliyotangulia nilimalizia kwa kuelezea maana ya neno Monsinyori au Monsinyo likimaanisha ni mtu anayefanya kazi katika ofisi ya askofu, akitekeleza majukumu ya kiaskofu japo hajafikia daraja hilo.

Tafsiri ya hilo neno niliitoa makusudi kwa kuwa matini yangu ya kwanza na ya pili niliyoipa jina HATUWEZI KUMTUPA KAMA MPAGANI ilimtaja mno marehemu Monsinyori Deogratiasi Mbiku ambaye zamani aliwahi kuwa paroko wa parokia kadhaa za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Mwanakwetu hilo nakumbuka sana kwani nikiwa mdogo wakati wa uhai wa Kadinali Lauriani Rugambwa, Padri Mbiku alikuwa paroko wa Parokia Chang’ombe jimboni humo, jirani na makutano ya Chang’ombe, karibu na Shule ya Sekondari Kibasila na Kituo cha Polisi cha Chang’ombe.

Kwa ramani za miaka hiyo Parokia ya Chang’ombe ilipakana na Parokia ya Mbagala na Parokia ya Kurasini.

Mwanakwetu nina hakika matini zangu mbili zimeeleza vizuri namna mzee wetu Kingunge Ngombale Mwiru na msimamo wake wa imani, nafahamu walio wengi walidhani kuwa Kingunge hakuwa na imani kabisa, binafsi ninaweza kusema alikuwa mtoro wa kanisani.

Natambua fika katika dunia yetu ya leo tabia ya utoro wa imani inafanywa na wengi sana na hata ile hoja ya kushangazwa kutaka kuhakiki uwepo wa Mungu, lakini pengine wengine wanapona katika hilo labda kwa kukaa nalo moyoni.

Nina imani wengi tutakuwa tumejifunza mno juu ya simulizi hii ya maisha ya kiimani ya Mzee Kingunge ambalo hilo ndilo nia ya kuandika matini haya.HATUWEZI KUMTUPA KAMA MPAGANI-II
Hayati Kingunge Ngombale Mwiru.

Walio wengi waliufahamu msimamo wa kiimani wa Hayati Kingunge Ngombale Mwiru kwa namna alivyokuwa akila kiapo.

Wengine wakisema kuwa huyu hana dini, wengine, wakisema Kingunge dini yake katiba. Haya yalisemwa mno katika uhai wake kila alipokuwa akila kiapo kwa nafasi alivyochaguliwa.

Nakumbuka kiapo chake cha mwisho mzee huu kilikuwa ni Ubunge wake katika Bunge la Katiba, kubwa kwa kuwa katika kila kiapo chake hakushika Biblia wala Korani.

Hoja hiyo binafsi ilinipa tafakari kubwa, je kitendo cha kuvishika vitabu hivyo vya dini katika kiapo cha nafasi za kiserikali ina maana kuwa wewe ni mfuasi wa imani hizo?.

Je hiyo nafasi unayokula kiapo unakwenda kuifanya kazi kwa misingi ya imani yako? Nako nyuma ya pazia ya mawazo yangu kukiwa na hoja juu ya nchi kutokuwa na dini.

Natambua fika majibu ya kushika vitabu hivyo yatakuwepo mengi kubwa ni kudhihirishia umma wewe ni wa upande gani wa imani, binafsi hilo sina shinda nalo lakini hoja ya msingi je wale wote wanaokula viapo kwa kushika vitabu hivyo vya dini je inapofikia wakati wa kuamua jambo lenye maslahi ya imani yake je wanasimamia imani zao? Kama wasipofanya hivyo je wanapaswa kuadhibiwa na imani zao?.

Walio wengi mbele kiapo cha cheo hicho utawaona wameshika biblia kwa ukakamavu mkubwa akiwa katika kuta za mahakama kama jaji anapofanya maamuzi anakuwa mpagani kidogo, Jumapili asubuhi biblia kwapani anakuwa mkristo. Akipanda cheo akienda kula kiapo biblia kwa ukakamavu inashikwa.

Naye mbunge yanakuwa yale yale anakula kiapo mbele ya spika biblia mkononi, lakini mnapojadili na kupitisha miswada ya sheria inayokiuka misingi ya dini yake anaiunga mkono . Jumapili ikifika anashika kwapani biblia yake.

Swali la kujiuliza je Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa sahihi kuapa katika shughuli za kiserikali kwa kutokutumia vitabu vya dini?.

Mwanakwetu kuna wakati Jimbo moja Katoliki la Marekani lilimualika Kadinali Francis Arinze kutoka Vatikani, kadinali huyu akiwa huko aliulizwa swali juu msimamo wa dini na maadili katika katika taifa hilo linaloamini kutenganisha baina ya dini na shughuli za serikali.

Kadinali Arinze akijibu swali hilo alisema kuwa yeye hakwenda Marekani kukosoa ule utaratibu wao wa kutenganisha baina dini na shughuli za kiserikali, lakini ndani yake jambo hilo lina tafsiri nzuri na tafsiri mbaya, akamalizia kwa kusema kuwa

“Walei wote tambueni kuwa hauwezi kujitenga na wajibu wako kama raia na wajibu wako kama mkristo.”

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news