NA DIRAMAKINI
JUMUIYA Wavuvi wa Eneo la Nyamkazi katika Ziwa Victoria wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera, wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwatambua wavuvi walioshiriki kuwaokoa abiria wa ajali ya Ndege ya Precision kwa kuwapa shilingi Milioni 10 pamoja na kuwawekea mazingira ya kupata mafunzo ya uokoaji.
Wakizungumza na waandishi habari mkoani Kagera, wavuvi hao, wamesema walifanya kazi ya kuokoa kwa kujitolea bila ya kutegemea malipo, lakini wamefurahia hatua ya Serikali kuwatambua wavuvi wote walioamua kujitoa maisha yao na kusaidiana na Serikali kuokoa maisha ya Watanzania.
Kwa upande wake Kiongozi wa Waislamu wa Wilaya ya Bukoba Mjini,Sheikh Yussuf Kakwekwe na Askofu. Dkt.Abednego Keshomshahara wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi wa Kanisa la K.K.K.T Bukoba wamesema vitabu vyote vya dini vinaeleza Mamlaka za Serikali zinavyoweza kushirikiana na Wananchi hususani kwenye kuokoa maisha ya watu wengine, na wakatumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kuwatambua wavuvi waliojitolea kushirikiana na Serikali kuwaokoa wahanga wa ajali Ndege kwa kuwapatja Milioni 10, mafunzo ya uokoaji na kuwaahidi mikopo ya Boti za Kisasa.
Akizungumza kwa niaba ya Machifu Mkoa wa Kagera, Chifu wa Mkoa huo Chifu. Hermes Nyarubamba amesema ushirikiano uliooneshwa kati ya wananchi na Serikali unapaswa kudumishwa, ili kuweka mazingira ya kushirikiana tena hasa wakati wa majanga kama ambavyo mila na tamaduni za kitanzania zinawataka Watanzania kusaidiana.