NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.Stergomena Tax amepongeza uamuzi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wa kufungua Konseli Kuu (Ubalozi Mdogo) visiwani Zanzibar na kutoa wito kwa wananchi kutumia uwepo wa Konseli hiyo kuboresha ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, utalii na masoko kwa bidhaa za Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Visiwani Zanzibar, Mhe. Balozi Saleh Ahmed Alhemeiri. Hafla hiyo fupi imefanyika hivi karibuni katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar. Mhe. Dkt. Tax yupo mjini Zanzibar kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Mabalozi wa Tanzania unaoendelea mjini hapo kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022.
Mhe. Dkt. Tax ametoa pongezi hizo hivi karibuni wakati akipokea
Hati za Utambulisho za Konseli Mkuu wa UAE, Zanzibar Mhe. Balozi
Saleh Ahmed Alhemeiri katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar.
Amesema
hatua hiyo ni muhimu sana katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria
uliopo kati ya Tanzania na UAE kwani sasa fursa nyingi zilizopo
Zanzibar ikiwemo utalii, uchumi wa buluu na biashara vitashamiri zaidi
na kukua.
Mhe. Dkt. Tax akizungumza na Mhe. Alhemeiri mara baada ya kupokea hati za utambulisho. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Tax alipongeza uamuzi wa Serikali wa kufungua Konseli Kuu Zanzibar na kutoa wito kwa watanzania kutumia uwepo wa Ofisi hiyo kuimarisha ushirikiano
Ameongeza kusema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Awamu ya Nane ya Zanzibar chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
zimeendelea kuimarisha ushirikiano na nchi mbalimbali pamoja na kutafuta
fursa za biashara, utalii, uwekezaji na
masoko kwa bidhaa za Tanzania ili kuiwainua kiuchumi watanzania wote.
Ameongeza
kwamba kufunguliwa kwa Konseli Kuu hiyo ni matokeo ya ziara mbalimbali
za viongozi hao nchini humo ikiwemo ile ya Mhe. Rais Samia aliyoifanya
nchini UAE mwezi Februari 2022 wakati wa Maonesho ya Biashara ya
Kimataifa ya Dubai Expo 2020.
Pia amesema wakati wa ziara hiyo, pamoja na mambo
mengine,Mikataba na Hati za Makubaliano mbalimbali zilisainiwa kwa
ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa
nchini.
“Napongeza kwa dhati uamuzi wa Serikali ya UAE wa
kufungua Konseli Kuu au Ubalozi mdogo hapa Zanzibar. Ni imani yangu
kuwa, uwepo wa Konseli Kuu hii utasaidia kuharakisha utekelezaji wa
masuala mbalimbali ya ushirikiano ambayo tayari yamekubalika kwa manufaa
ya pande hizi mbili,"amesema Dkt. Tax.
Akitaja maeneo ya
kipaumbele ya ushirikiano kwa upande wa Zanzibar, Mhe. Waziri Tax
amesema ni pamoja na Uchumi wa Buluu hususan katika uvuvi wa bahari kuu,
utalii, biashara na uwekezaji kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Alhemeiri wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza (kulia) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mariam Mrisho (kushoto).
Pia Mhe. Dkt Tax amemhakikishia ushirikiano Balozi huyo na kwamba ana imani kuwa kupitia yeye masuala mengi yatakamilika.
”Tutashirikiana
na wewe kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizi mbili
hususan kwa upande wa Zanzibar yanatekelezwa na kama ulivyosema awali
kwa kiasi fulani Zanzibar inafanana na Dubai, basi tujielekeze kuigeuza
Zanzibar kuwa Dubai ya Afria,"amesema Dkt. Tax.
Kwa upande
wake, Mhe. Alhemeiri amesema amefarijika kuwepo Zanzibar na kwamba yupo
tayari kushirikiana na Serikali hiyo katika kukuza biashara, kilimo,
elimu, na uchumi wa buluu kwani zipo fursa lukuki katika Kisiwa hiki
zinazohitaji kuendelezwa.
“Nia yetu ni kushirikiana na Serikali kukiendeleza Kisiwa kizuri cha
Zanzibar. Nimeona zipo fursa nyingi za kufanyia kazi. Nitajikita zaidi
kwenye masuala ya utalii, biashara, elimu, uchumi wa buluu na
usafirishaji kwa kuzishawishi mamlaka za UAE kuongeza safari za moja kwa
moja za Mashirika ya Ndege ya UAE kuja Zanzibar ili kukuza utalii,"
amesema Mhe. Alhemeiri.
Mhe. Dkt. Tax yupo jijini Zanzibar kwa
ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania unaofanyika
Kisiwanii humo kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022.