NA INNOCENT NATAI
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia,Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) amewataka vijana wa kitanzania kujenga utamaduni wa kujiajiri na kuwa wabunifu ili kuisaidia Serikali kupunguza kundi la wasio na ajira.

Waziri Mkenda amesema kuwa, mpaka sasa Serikali imepiga hatua kubwa katika kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri ambapo uzinduzi wa kampuni hiyo inayojihusisha na masuala ya habari, kijana Mtanzania amewekeza hivyo ameongeza chachu kwa vijana wengine kuona ni namna gani wanaweza kuajiriwa huku wamejiajiri na kuajiri vijana wengine.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Mhandisi Mathew Kundo amempongeza Mtendaji Mkuu wa WazoHuru Media Group Limited, Mathias Canal kwa kuhakikisha anafuata sheria na kanuni za uanzishwaji wa Kampuni na Kituo cha Habari kama yalivyo matakwa ya kisheria.

Pia ameongeza kuwa, amefurahishwa na kuona kijana wa kitanzania anajiajiri na kuweza kuajiri vijana wengine ili kuhakikisha wanajipatia kipato na kuwezesha upatikanaji wa habari na elimu kwa jamii kwa urahisi.

Ameongeza kuwa, mpango wa kampuni hiyo iliyojipambanua katika masuala ya Habari na mawasiliano ilianza kupitia kundi la WhatsApp Mkoani Iringa mwaka 2014 na baadae kuanzisha televisheni ya Mtandaoni (Youtube Tv) pamoja na Blog.
Canal amesema kuwa, malengo ya kampuni hiyo ni pamoja na kuanzisha gazeti litakalofahamika kama WazoHuru, kuanzisha kituo cha redio itakayofahamika kama WazoHuru Fm na Televisheni itakayofahamika kama WTV.