NA MATHIAS CANAL-WEST
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof.Adolf Mkenda (Mb) pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed wameongoza kikao cha kazi cha mapitio ya Sera na Mitaala.


Waziri Mkenda amesema kuwa, kabla ya mkutano wa wadau wa elimu nchini pia kutakuwa na mkutano wa kazi wa Baraza la Mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara zote ili kujadili kwa kina kuhusu mustakabali wa sekta ya elimu na mapendekezo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu sekta ya elimu nchini.


"Sisi Mawaziri tumepewa maagizo ya kuhakikisha tunasimamia mabadiliko haya ya sera na mitaala bila kupishana, hata kama wale wanakuwa wakiogelea kule baharini na hawa wanakulia kwenye milima na kwenye madini lakini mwisho wa siku yule mvuvi na yule muwindaji wawe katika lugha moja katika mifumo yetu,"amesisitiza Mhe.Lela
.
Kadhalika, Waziri Lela amepongeza kwa wadau kutoka pande zote mbili za Muungano kushirikishwa katika mapitio ya sera na mitaala kwani mjadala huo pia unasaidia kamati ya Zanzibar katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema kuwa, mpaka sasa maoni yote yanayokusanywa bado ni mali ya wizara kabla ya mapendekezo ya serikali kwa ujumla ambayo inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa upande wa Zanzibar ambaye tayari ameridhia kupitishwa katika hatua zilizofikiwa.