Waziri Mkuu aagiza Jiji la Dodoma, LATRA kukutana

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jiji la Dodoma ukutane na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) ili kutengeneza mpangilio safari za daladala ndani ya jiji hilo kuelekea soko jipya la wajasiriamali wadogo lililoko barabara ya Bahi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua eneo la kuuzia mboga, viungo na matunda katika Soko Kuu la Wafanyabiashara Wadogo lililopo Bahi Road jijini Dodoma, Novemba 24, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema sambamba na utekelezaji wa maagizo hayo Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanafanya maboresho ya stendi iliyoko katika eneo hilo ili iweze kukidhi viwango vya kupokea magari ya abiria yatakayoelekezwa eneo hilo.

Ametoa maagizo hayo Novemba 24, 2022 mara baada ya kukagua soko jipya la wajasiriamali wadogo lililoko Bahi Road jijini Dodoma.

Pia ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma isimamie utoaji wa fedha za mikopo kwa wafanyabiashara katika soko hilo ili waongeze mitaji na kukuza biashara zao. “Nataka nipongeze uamuzi wenu wa kuja hapa mmefanya maamuzi sahihi na mtanufaika.”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ni dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuwainua wafanyabiashara kwa kufungua milango ya ufanyaji biashara kwa uwazi na Serikali kuwapa huduma muhimu zitakazowasaidia kuleta tija kwenye shughuli zao.

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha anafanyia kazi changamoto zilizojitokeza baada ya wafanyabiashara kuhamia katika eneo hilo ikiwemo kuboresha barabara, vikingia mvua, taa za barabarani pamoja na kushirikiana na TARURA kuweka taa za barabarani.

Awali akijibu maombi ya wafanyabiashara hao, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema Halmashauri ya Jiji imetenga Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kutoa mikopo midogo kwa wafanyabiashara walioko na hadi kufikia mwezi disemba mwaka huu watakuwa wameshakamilisha taratibu za utoaji wa mikopo hiyo.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Festo Dugange amesema ujenzi wa soko hilo ni dhamira njema ya Rais Samia Sulluhu Hassan ya kuwajali na kuwapenda wafanyabiashara wadogo wadogo waondokane na adha ya kutembea na bidhaa zao badala yake wapate sehemu nzuri na bora ya kufanya biashara zao.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wadogo Mkoa wa Dodoma Bw. Chrisrian Mohamed Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za kujenga soko hilo ambalo litafungua fursa kwa wajasiriamali hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news