NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri nchini kuongeza umakini katika manunuzi ya vifaa vinavyotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili iweze kukamilika katika muda uliopangwa na kutoa huduma kwa wananchi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua maji wakati alipokagua ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Kisarawe akiwa katika siku ya tatu ya ziara ya Mkoa wa Pwani, Novemba 29, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Ametoa wito huo Novemba 29, 2022 alipozungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Wenyeviti wa Halmashauri wanapaswa kuwa wakali katika kufuatilia manunuzi ya vifaa mbalimbali na watumie wakaguzi wa ndani katika kufuatilia taarifa za manunuzi.
“Manunuzi hapa kisarawe ni ya gharama kubwa katika miradi yenu, miradi haishi kwasababu ya gharama kubwa, na bahati mbaya mnafanya hivyo kwa fedha za Serikali kuu” .
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumfuatilia aliyekuwa afisa mapato katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Fredy Bandai aliyehamishiwa Mtwara vijijini “Huyu asimamishwe kazi na arejeshwe Kisarawe ili aje atolee taarifa ya fedha kiasi cha shilingi milioni 253 alizokusanya lakini hazionekani”.
Pia, Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe James Chitumbi kwa kukiuka maadilin ya uongozi.
Kadhalika Waziri Mkuu amewataka wakuu wa Idara kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao “Tunataka watanzania wahudumiwe, ninyi watumishi wa umma ni wahudumu kwa wananchi wetu, fuatilieni miradi ili iweze kuleta tija kwa wananchi”
Awali akikagua mradi wa maji Kisarawe mjini, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya maji na kuviingiza kwenye mfumo.
Amesema kuwa, licha ya kuongezeka kwa kiwango cha maji kwenye mfumo wa uzalishaji na usambazaji, wasilale bali waendelee kuwatumia wataalam wa ndani kutafuta maji zaidi.
Amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la makazi, viwanda na shughuli mbalimbali za kijamii ambazo kwa kiasi kikubwa zinahitaji uwepo wa maji ya kutosha. “Tusilale tuendelee na uzalishaji wa maji, Tunataka huduma hii isambae na iwafikie watu wote”
“Ndugu wafanyakazi wa DAWASA mnapaswa kutambua maji ni huduma nyeti kwenye maisha ya binadamu, kazi yenu inahitaji uaminifu na uadilifu mkubwa, fanyeni kazi hii ya umma, wahudumieni watanzania, tambueni maeneo yenye uhitaji na mpeleke huduma”
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt Festo Dugange amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepekea zaidi ya shilingi bilioni 6 katika halmashauri ya wilaya ya kisarawe kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na ukarabati mkubwa wa hospitali ya wilaya.