Waziri Mkuu azindua ugawaji wa Vishikwambi kwa Sekta ya Elimu

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Ijumaa Novemba 4, 2022 amezindua ugawaji wa vishikwambi katika sekta ya elimu na amesisitiza kwamba vifaa hivyo vitumike katika kuboresha mchakato wa utoaji elimu ili kuinua ubora wa elimu nchini na si vinginevyo.
Akizindua ugawaji wa vishikwambi hivyo katika ukumbi wa mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mtumba, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali haitarajii kuona vitendea kazi hivi vinazagaa mtaani na pengine kumilikishwa kwa wasiohusika.

Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la ugawaji wa vishikwambi hivyo kwa walimu wote nchini ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa njia ya TEHAMA, hivyo ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iimarishe ufundishaji wa somo hilo katika ngazi zote za elimu.
Pia, Waziri Mkuu amezielekeza mamlaka zote zinazohusika katika zoezi la ugawaji wa vifaa hivyo zihakikishe vinawafikia walengwa wote kwa wakati ili vifanye kazi iliyokusudiwa. “Hapa ningependa kusisitiza kuwa vishikwambi hivi ni kwa walimu tu na kweli viwafikie na kutumika na walimu na si vinginevyo.”

“Viongozi wote mtakaokuwa na jukumu la kugawa vishikwambi hivi hakikisheni hakuna mwalimu atakayekosa kishikwambi. Ninataka niwakumbushe tu kwamba idadi ya walimu na idadi ya vishikwambi tunazijua.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka walengwa wote wahakikishe wanatunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa malengo kusudiwa ikiwemo kusaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa zana mbalimbali za kufundishia na kujifunzia (rejea) kwa walimu.

Waziri Mkuu amesema Serikali Awamu ya Sita inayoongozwa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa vitendo kuwekeza katika eneo la TEHAMA ili kuwawezesha vijana kupata ajira na kuzalisha ajira na kukuza uchumi kupitia teknolojia.
Amesema azma hiyo ya Serikali inakwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 ambayo inaielekeza Serikali kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ngazi mbalimbali za Elimu kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya watu kwa ujumla.

Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alisema walengwa wa vishikwambi hiyo ni walimu na wakufunzi waliopo katika Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu, Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Wadhibiti Ubora wa Shule na Maafisa Elimu wa ngazi ya Mkoa, Halmashauri na Kata.

Alisema vishikwambi 293,400 ambavyo vilitumika katika zoezi la sensa ya watu na makazi kwa upande wa Tanzania Bara vitagawiwa kwa walimu wa shule za msingi za umma (185,404), walimu wa shule za sekondari za umma (89,805), wadhibiti ubora wa shule ngazi ya wilaya ya kanda(1,666).
Wengine ni wakufunzi wa vyuo vya ualimu vya umma (1,353), vyuo vya maendeleo ya wananchi-FDC (297), Maofisa Elimu Ngazi ya Mkoa, Wilaya na Kata (5,772), Wakufunzi wa Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi-VETA (996) na Baraza la Mitihani la Tanzania-NECTA(8,357).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news