Waziri Prof.Mkenda:Mageuzi ya elimu yanayokuja yanakwenda sambamba na ujuzi

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yanayokuja yanakwenda sambamba na kuandaa mazingira ya kuhakikisha elimu ujuzi inapatikana.
Mhe. Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja cha Menejimenti ya Wizara na ile ya VETA chenye lengo la kujadili kwa pamoja mikakati ya utekelezaji wa ujenzi wa VETA 63 za wilaya na moja ya mkoa.
Amesema, moja ya eneo linaloangaliwa katika kutoa elimu ujuzi ni kupitia vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) hivyo ni vizuri kuwa na mikakati thabiti ya kuhakikisha VETA 63 za Wilaya na moja ya mkoa ujenzi unaanza.

"Nataka twende pamoja, katika kuweka historia hii; tunakwenda kufanya mageuzi makubwa ya elimu kwa kuhakikisha tunatoa elimu ujuzi, sasa kazi ya mapitio ya Sera na Mitaala inakwenda vizuri na tuko tayari kufanya wasilisho kwa ajili ya mjadala wa Kitaifa, sasa nataka huku kwenye ujenzi wa VETA 63 ambako elimu ujuzi inapatikana kuende kwa kasi na kwa wakati ,"amesema Prof. Mkenda.
Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa VETA hizo hivyo kutaka mkakati wa kuhakikisha ujenzi unaanza mapema na kujengwa kwa usahihi kwa kuzingatia taratibu zote husika.

Akizungumzia ujenzi wa Kampasi za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 kupitia Mradi wa HEET Mhe. Mkenda amewataka Wakandarasi waliopo wizarani kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji na kushirikiana na na Vyuo Vikuu kujua mikakati iliyowekwa na Vyuo mama kuhusu ujenzi huo ili kazi iweze kwenda kwa haraka.
Akizungumzia maandalizi ya ujenzi wa VETA hizo Mhandisi George Sambali kutoka VETA amesema mpaka sasa kati ya wilaya 63 zinazojengewa VETA wilaya 59 tayari zina maeneo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news