NA MWANDISHI WETU
WATU 57 wamenusurika kifo katika ajali iliyotokea Barabara Kuu ya Morogoro - Dar es-Salaam baada ya basi la abiria la Kampuni ya Al-Seady lililokua linatoka Kilosa kuelekea Dar es Salaam kupinduka eneo la Kitungwa Manispaa ya Morogoro.
Ajali hii imetokea ikiwa imepita siku tatu tangu kutokea ajali ya IT na Lori la Mafuta eneo la Iyovi Mikumi Barabara ya Morogoro - Iringa na kuua watu watano wakiwemo wanandoa wawili.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi la Ally's Star lililokua linatokea Dar es salaam kuelekea Mwanza kutaka kuyapita magari yaliyopo mbele yake bila kuchukua tahadhari.
Ndipo dereva wa gari la Al Saedy alimkwepa kuepusha gari kugongana uso kwa uso ndipo likapinduka, hata hivyo dereva aliyesababisha ajali hiyo anashikiliwa na jeshi la polisi.
Kaimu Kamanda wa Jeshi za Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Emanuel Ochieng amesema abiria 17 wamepata majeraha madogo na jeshi hilo limewapatia huduma ya kwanza na kuendelea na safari.
Amesema,Kondakta wa basi hilo amekimbizwa hospitali ya Rufaa Mkoa Morogoro kupata matibabu zaidi baada ya kupata majeraha makubwa.