Amir wa Qatar ampa kongole Mfalme wa Morocco kwa timu yake kutinga nusu fainali Kombe la Dunia

NA DIRAMAKINI

AMIR wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani jioni ya Desemba 10, 2022 amempigia simu kaka yake, Mfalme Mohammed VI wa Ufalme wa Morocco kumpongeza kwa ushindi mkubwa wa timu ya taifa ya Morocco na kusonga mbele kwao nusu fainali ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Qatar 2022.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na The Peninsula ikifafanua kuwa, kiongozi huyo amefurahishwa na matokeo hayo ambapo Morocco wameibuka kuwa timu ya kwanza ya Kiarabu na Kiafrika kufika hatua hiyo katika historia ya michuano hiyo.

Youssef En-Nesyri wa Morocco akifunga bao la kwanza la timu hiyo kwa kichwa. (Picha na Francois Nel/Getty Images).

Vijana hao wa Walid Regragui wameweka historia kwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika na katika ulimwengu wa Kiarabu kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kwa kuitoa Ureno.

Timu hiyo ya Ureno ambayo inaundwa na mastaa wakubwa Duniani akiwemo Cristiano Ronaldo imechapwa na Atlas Lions bao 1-0 katika Uwanja wa Al Thumama mjini Doha.

Dakika ya 42, Youssef En-Nesiry alitumia vyema krosi ya Yahya Attiat-Allah kwenye eneo la hatari na mshambuliaji huyo wa Morocco akafunga bao kwa kichwa huku Diogo Costa akikosa cha kufanya..

Mafanikio ya Morocco ni kati ya ndoto ambazo hazikuwa zinafikirika kwa mashabiki na wapenzi wa soka barani Afrika.

Baada ya kutoka hatua ya makundi wakiwa mbele na kuwaondoa Uhispania katika mzunguko wa nane kupitia mikwaju ya penalti, lolote liliwezekana kwa vijana wa Regragui. Ingawa, Ureno ilipewa tangu hapo awali nafasi ya kushinda mchezo huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news