Argentina yatinga fainali kwa kuizamisha Croatia mabao 3-0

NA DIRAMAKINI

TIMU ya Taifa ya Argentina imeshinda mabao 3-0 dhidi ya Croatia siku ya Jumanne na kutinga fainali ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022.
Lionel Messi wa Argentina (10) na Mateo Kovacic wa Croatia wakiwania mpira wakati wa mechi ya nusu fainali ya soka ya Kombe la Dunia ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 kati ya Argentina na Croatia kwenye Uwanja wa Lusail mjini Lusail, Qatar, Jumanne ya Desemba 13, 2022. (Picha na AP).

Kupitia mtanange huo wa nguvu Desemba 13, 2022 Argentina walipata penalti baada ya Julian Alvarez kuangushwa na kipa wa Croatia Dominik Livakovic kwenye Uwanja wa Lusail nchini Qatar.

Lionel Messi alifunga mkwaju wa penalti dakika ya 34. Baada ya dakika tano, Argentina walipata bao la pili wakati fowadi Alvarez alipomalizia kwa shuti kali.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa mabao 2-0 kwa upande wa Albiceleste. Dakika ya 69, Messi aliwapiga chenga walinzi wa Croatia na kumkuta Alvarez akiwa eneo la hatari.

Alvarez alipiga shuti la mguu wa kulia kutoka kwenye eneo la hatari na kumshinda Livakovic, na kufanya matokeo kuwa mabao 3-0.

Wakati huo huo, kocha msaidizi wa Croatia Mario Mandzukic alioneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika dakika ya 35.

Pia, Messi alimshinda gwiji Gabriel Batistuta na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Argentina akiwa na mabao 11 kwenye Kombe la Dunia.

Kwa matokeo hayo, Argentina itamenyana na mshindi wa mechi ya Ufaransa na Morocco. Fainali itachezwa kwenye Uwanja wa Lusail siku ya Jumapili.

Aidha, kwa matokeo haya, Messi alitinga fainali ya pili ya Kombe la Dunia katika maisha yake ya soka. Katika fainali ya Kombe la Dunia 2014, Argentina ya Messi ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Ujerumani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news