Balozi Celestine Joseph Mushy kuzikwa wiki ijayo Kibosho

NA DIRAMAKINI

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na familia ya marehemu Balozi Celestine Joseph Mushy imesema, inaendelea na mipango ya maandalizi ya mazishi ambapo mwili wa marehemu Mushy unatarajiwa kuzikwa Desemba 20, 2022.

Ni maziko ambayo yanatarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Sambarai, Kata ya Kindi, Tarafa ya Kibosho, Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 16, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwili wa Balozi Mushy utasafirishwa kesho Jumamosi Desemba 17, 2022 kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwenda Moshi kwa ajili ya maandalizi ya mazishi yatakayofanyika siku ya Jumanne.

Balozi Mushy alifariki dunia Desemba 12, 2022 katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Mkata wilayani Handeni mkoa wa Tanga baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana na lori la mizigo na kuungua moto.

Aidha,Balozi Mushy aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria na Mwakilishi wa Kudumu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa Vienna, mwezi Januari 2022.

Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu Balozi Celestine Mushy mahali pema, Amina.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news