NA GODFREY NNKO
BALOZI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China,Mheshimiwa Mbelwa Kairuki ametambulisha mvinyo wa Tanzania katika soko la China.
Mheshimiwa Kairuki amefanya utambulisho huo Desemba 21, 2022 katika Mkutano wa Alcohol Innovation and Investment Conference 2022 uliofanyika jijini Hainan, China.
Hatua hiyo inawapa sababu nyingi wakulima wa zabibu na watengenezaji wa mvinyo hapa nchini kutabasamu, kwani mvinyo wa Tanzania unaingizwa katika soko la China ambalo linakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya bilioni moja.
“Tanzania ni nyumba ya ukanda mkubwa zaidi wa mvinyo Kusini mwa Jangwa la Sahara,”ameeleza Balozi huyo wakati akitambulisha mvinyo unaozalishwa nchini.
Pia amesema, uhusiano baina ya Tanzania na China umeboreshwa hadi kufikia ubia wa kimkakati kutokana na safari ya kihistoria iliyofanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan katika nchi hiyo yenye nguvu za kiuchumi duniani.
Aidha, Balozi Kairuki baada ya kuzindua bidhaa hiyo alionekana kuwa na matumaini kuwa, Tanzania itapokea wawekezaji zaidi siku za karibuni kutoka China ili kukuza sekta hiyo.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache duniani ambayo yanatajwa kuzalisha mvinyo wenye viwango bora ambao unatokana na ladha ya asili. Na Serikali imeweka mkazo mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa hiyo ili iweze kukidhi mahitaji ya ndani na nje kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu.
Novemba 5, 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alizindua tamasha la mvinyo mkoani Dodoma na kusisitiza kuwa uzalishaji wa miche ya zabibu za matunda uongezwe ili wajasiriamali wapate bidhaa kutoka mkoa huo.
“Hizi zabibu zinazouzwa barabarani siyo za kula kama matunda, hizo ni za mvinyo. Tuweke juhudi ya kuzalisha miche ya zabibu za mezani ili wajasiriamali wanaouza zabibu kwenye stendi za mabasi wapate bidhaa kutoka hapa Dodoma,”alisema Waziri Mkuu.
Alitoa wito huo wakati akizungumza na wananchi na wadau wa zao hilo waliofika kwenye uzinduzi wa tamasha la mvinyo kwenye viwanja vya Mashujaa jijini Dodoma.
“Tunataka miche ya zabibu kwa ajili ya mvinyo na ile ya kula izalishwe kwa wingi. Hivyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa itenge maeneo ya kuzalisha miche bora na kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja (Block farms) ili kuongeza uzalishaji na kurahisisha utoaji wa huduma za ugani, mitaji na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya mvinyo,"alielekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Pia alizitaka Sekretarieti ya Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zishirikiane na Wizara ya Kilimo kusimamia mikataba ya kilimo inayosainiwa baina ya wakulima, wanunuzi wa mazao na watoa huduma wengine ili kuhakikisha wakulima hawadhulumiwi.
Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Kilimo iratibu maonesho ya zabibu ili tamasha hilo liwe rasmi. “Mratibu wa tamasha hili, Bi. Atwite Makweta asaidiwe na wizara kusimamia maandalizi na kuanzia sasa haya maonesho yawe ya kudumu na yafanyike kila mwaka hapa Dodoma.”
Siku hiyo,akizungumza kwa niaba ya wasindikaji wa zao hilo, Mkurugenzi wa kampuni ya Alko Vintage, Bw. Archard Kato alisema zao la zabibu lilianza kuzalishwa mwaka 1959 ambapo hadi kufikia mwaka 2005, wadau mbalimbali wakiwemo DOWICO, TAVICO, ALKO VINTAGE na CETAWICO wamekuwa wakiliendeleza kwa hatua tofauti na kufikia vijiji 93.
“Sasa hivi tumefikisha viwanda 15 kutoka viwanda saba vilivyokuwepo mwaka 2020. Na hivi ni vidogo, vya kati na vikubwa. Tunakabiliwa na changamoto ya ubora wa zabibu kutokana na ukosefu wa utaalamu, nyenzo duni kwa wasindikaji na tunahitaji mafunzo zaidi kwa wakulima na wasindikaji ili kuboresha zao hili,”alisisitiza.