NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka Watanzania kupuuza taarifa hii hapa chini wanayohusishwa nayo kuhusu kujikuza kama wanadada kupitia Forex, hii ni taarifa batili ambayo inatokana na watu wenye nia ovu.
BoT, imesema taarifa hii haina ukweli wowote na huenda imeandaliwa kwa ajili ya kuwalaghai wananchi, hivyo kila mmoja anapaswa kuipuuza.
Benki Kuu ya Tanzania ina mamlaka ya kutoa leseni, kudhibiti na kusimamia benki na taasisi za fedha zikiwemo benki za biashara, taasisi za huduma ndogo za fedha, benki za jamii, benki za maendeleo, kampuni za karadha, taasisi za mikopo ya nyumba, watoa huduma ndogo za fedha, taasisi za taarifa za wakopaji, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na ofisi za uwakilishi za benki zilizoko nje.
Pia, Benki Kuu ina wajibu wa udhibiti na usimamizi wa masuala ya kifedha (uwekezaji) wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini Tanzania. Jukumu la msingi katika udhibiti na usimamizi wa taasisi za fedha ni kuhakikisha kuna uthabiti, usalama na ufanisi wa mfumo wa fedha na kupunguza uwezekano wa wenye amana kupata hasara.
Aidha, taarifa rasmi za Benki Kuu ya Tanzania mara zote huwa zinachapishwa katika tovuti rasmi ya benki; https://www.bot.go.tz ikiwemo mitandao yake ya kijamii ya Twitter https://twitter.com/BankOfTanzania Instagram https://www.instagram.com/bankoftanzania_/ Facebook https://web.facebook.com/BankOfTanzaniaOfficial