NA ADELADIUS MAKWEGA
MWANAKWETU anazaliwa kwa Baba Mkatoliki na kwa mama yake Muangalikana. Kwa baba yake ndugu huyu hatua kubwa sana ya imani ni Ukatekista na kwa mama yake hatua kubwa waliofikia ni wameanzia katika Uchungaji na baadhi kufikia Ukanoni.
Kanoni ni sawa Mosinyori ambaye ni mtu anayefanya kazi katika ofisi ya Askofu akitekeleza majukumu ya kiaskofu japo hajafikia daraja hilo.
Mwanakwetu tangu anazaliwa amekuta nduguze wanasherekea sikukuu ya Noeli ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo miaka zaidi 2000 iliyopita.
Msomaji wangu unaweza kujiuliza leo mwanakwetu kawa katekista au kavaa kanzu la unjilisti la hasha hajajaliwa nafasi hizo. Mwanakwetu ni mtu mdogo sana. Kutokana na Mwanakwetu kuokota okota kutoka kwa nduguze makatekista, wachungaji na makanoni katika imani hii ya Kikristo leo hii anataka akwambie jambo moja zuri nadhani si wengi wanalolifahamu.
Sote tunafahamu kuwa Yesu Kristo alizaliwa katika Mji wa Daudi unaofahamika kama BETHLEHEM. Bethlehem ni jiji lililopo huko Palestina umbali wa kilomita 10 sawa na maili kama sita Kusini mwa Yerusalem.
Umbali huo kwa Tanzania kama ni Dar es Salaam ni kutoka Mbagala Mpili hadi Magomeni Mapipa au kwa Jiji la Dodoma ni sawa na kutoka Makole hadi Nzuguni.
Jiji la BETHLEHEM linakadiriwa kuwa na wakazi 25,000 na shughuli yao kubwa ambayo inawaingizia kipato ni utalii hasa kipindi cha sikukuu ya Noeli. Utalii wa BETHLEHEM unaliingizia jiii hilo asilimia 65 ya mapato yote kwa mwaka na BETHLEHEM pekee inaingiza asilimia 11 ya mapato yote yote ya mamlaka ya Palestina.
Mji huu unatajwa miaka mingi tangu 1350- 1330 kabla ya Kristo Kuzaliwa, ukitajwa kama mji wa watu wa Kanani. Huku mji huo ukipitia changamoto nyingi za vita na kubomolewa na kujengwa tangu enzi.
Katika Agano Jipya Injili ya Luka inasema kuwa Wazazi wa Yesu walisafiri kutoka Nazareth kwenda Bathlehem ambapo hapo Yesu alizaliwa. Injili ya Matayo inautaja MJI wa BETHLEHEM kama ni mji aliyozaliwa na ikiongeza kuwa mfalme Herode aliambiwa kuwa Mfalme wa Wayahudi amezaliwa katika mji huo.
Picha na Enjoybethlehem.
Hilo likamtia shaka mheshimiwa huyu, duu kutakuwepo wafalme wawili katika mji huu? Mafahari wawili hawakai zizi moja, hapo ndipo akaagiza kuuwawa kwa watoto wote wa kiume katika mji wa BETHLEHEM waliokuwa na umri kuanzia siku moja hadi miaka miwili na balaa lilipoanza wazazi wa Yesu walikimbia BETHLEHEM na kwenda Misiri.
Neno BETH LEHEM jina linalomaanisha NYUMBA YA MKATE. Katika neno BETHLEHEM pana maneno mawili ya Kiebrania BET/BEIT na LEHEM/LECHEM ikimaanisha BET/BEIT- NYUMBA na LEHEM/LECHEM -MKATE.(Maandishi BEIT na LECHEM namna yanavyotamkwa)
Kwa wasomaji wa Bibilia kitabu cha Mika 5.2 kinasema hivi,“Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye asili yake imekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.”
Hayo ya Mika na katika Injili ya Yohane 6.35 inasema hivi,“Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.”
Mwanakwetu upo?
Kumbuka asilimia 65 inayoliingizia Jiji la BETHLEHEM kwa utalii na kumbuka asilimia 11 ya uchumi mzima wa Mamlaka ya Palestina unatokana na uchumi wa BETHLEHEM. Je wewe mwanakwetu ulipozaliwa uwepo wako duniani unasaidia kuwaingizia nduguzo chochote katika uchumi wao?.
Hoja siyo kukaa duniani milele bali kufanya mambo yatakayodumu milele kama ilivyo sasa BETHLEHEM kuwa nyumba ya shibe.Nakutakia noeli na mwaka mpya mwema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257