BURIANI JOACHIM KAPEMBE

NA ADELADIUS MAKWEGA

MARA baada ya Rais John Magufuli kushinda uchaguzi wa mwaka 2015 alichelewa sana kuunda Baraza la Mawaziri lakini baadaye aliunda baraza hilo akimchagua mheshimiwa Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mara moja, alipoteuliwa ndugu huyu alianza ziara za kuzunguka katika taasisi na vyombo vilivyo chini ya iliyokuwa wizara hiyo.

Mheshimiwa huyu alienda TBC BH iliyokuwa TBC Makao Makuu Tazara Dar es Salaam na kufanya kikao na menejimenti ya TBC, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Clement Mshana alimwambia Waziri Nnauye kuwa yeye amewaalika viongozi wa wafanyakazi katika kikao hicho kwa heshima yao na kuheshimu uongozi huo kwani yeye mwenyewe Mkurugenzi Mshana aliwahi kuwa Katibu wa chama cha Wafanyakazi wa iliyokuwa RTD.

Mwanakwetu mwenyekiti wa wafanyakazi TBC Makao Makuu wakati huo aliingia huku TBC Mikocheni aliingia ndugu Joachim Kapembe aliyekuwa Katibu wa Chama cha Wafanyakazi TBC Mikocheni.

Yalizungumzwa mengi kikaoni hapo upande wa menejimenti ya shirika hilo nao wawakilishi wafanyakazi mwanakwetu na Kapembe na mwisho serikali ilizungumza na vyombo vya habari.

Baada ya kikao hicho mheshimiwa Nnauye aliwaalika viongozi kadhaa wa wafanyakazi TBC wizarani Dar es Salaam wakiongozwa na mwanakwetu na pia mtangazaji mkongwe wa wakati huo (RTD na TBC) Malima Ndelema,

Miezi kadhaa nyuma kabla ya kikao hicho TBC ilifanya uchaguzi wa viongozi wake wa chama cha wafanyakazi ambapo Joachim Kapembe alichaguliwa kuwa katibu wa wafanyakazi TBC Mikocheni nako TBC BH katibu akichaguliwa Othumani Idd na mwanakwetu akichaguliwa mwenyekiti.

Wakati huo Joachim Kapembe akiwa miongoni mwa wafanyakazi wapya waliajiriwa na TBC miaka michache baada ya kuundwa na pia akiwa miongoni mwa wanachama wa SACCOS ya wafanyankazi naye mwanakwetu akiwa mwanachama wa RTD SACCOS.

Baadaye Joachim Kapembe aliamua kuhamia TBC Tanga ili awe jirani na nyumbani kwao huku maombi haya ya uhamisho wake yalikubalika haraka sana wengi wakijiuliza kwa nini anahama alikuwa tayari ni kiongozi wa wafanyakazi aliyetegemewa sana?.

Mwenyewe alikiri kuwa maombi aliomba mapema kabla ya kuchaguliwa hivyo hakuwa na budi kuhama kwa kuwa maombi hayo yalikubaliwa.

Mwanakwetu alipangiwa majukumu huko Lushoto -Tanga huku wakati huo huo Kapembe akifanya kazi kama mpiga picha.

Ndugu huyu baadaye alianza kuripoti na siyo kuwarekodi wengine hilo likiwa jambo jema sana baada ya kumshirikisha Mama Martha Swai ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Matukio wa TBC wakati huo.

Mwanakwetu akiwa Lushoto alikuwa jirani mno na wanahabari Sophia Wakati (Uhuru), Mashaka Mhando (Majira) , William Mgazija (ITV &Radio One), Herman Mbonea(Star TC & Redio Free Africa)) walienda na Joachim Kapembe kuweza kumuunganisha tena na mwanakwetu, hapa mwanakwetu akiwaeleza kuwa anamfahamu sana ndugu huyu tangu TBC.

Huko ndugu Kapembe alifanya kazi vizuri sana akiripoti kazi kadhaa za maendeleo vijijini wakilala hadi vijijini katika mazingira magumu mno katika vijiji vya Tewe, Kishangazi, Mbaramo, Mrigirigi, Mabiri, Kikumbi, Makanka na Mhindulo hivi ni vijiji vyenye changamoto kadhaa katika Halimashauri ya Lushoto.

Baadaye mwanakwetu alihamishiwa Mbozi huko nako Joachim Kapembe na wenzake walikutana na mwanahabari Rose Magwe (Azam) na walifanya kazi hivyo hivyo kwa uhodari mkubwa katika vijiji vya Ndolezi, Msia, Ihanda, Namwangwa, Hezya, Isandula, Mponela, Bara, Namtunduru, Magamba, Utambalila, Nambizo, Shiwinga, Iporoto, Shilanga na Hantesya.

Mwanakwetu anakumbuka kuwa usiku mmoja walifika katika Kijiji cha Hantesya Kata ya Nyimbili Wilayani Mbozi na kulala katika nyumba mojawapo ya Kanisa la Moraviani Hantesya ili kudamkia kazi mbalimbali, madaktari na wauguzi waweze kutibu katika kliniki tembezi katika kata hiyo inayopakana na Wilaya ya Ileje.

Kanisa la Moravian Hantesya walitoa nyumba ya kulala kwa watumishi hao wakiwamo wanahabari hao na kulala mazingira hayo hadi asubuhi na kulipokucha huduma ya tiba na mikutano ya kuhamasisha maendeleo ilifanyika na matukio hayo kuripotiwa.

Wanakijiji cha Hantesya wapenda sana maendeleo walifurahi mno, huku nao msafara huo ukichangia mabati, rangi na mifuko ya saruji kwa kanisa hilo.

Joachim Kapembe hakulalamikia hilo akisema, “Jamani hawa ndiyo Watanzania wenyewe na ndugu zetu tufanye kazi kwa moyo wote.”

Mwanakwetu anakumbuka akiwa Lushoto na Mbozi Kapembe kila ilipofika Jumapili alishiriki ibada katika makanisa ya Kiangalikana katika miji hiyo mathalani pale Lushoto Kanisa la Mtakatifu George na pale Mbozi kanisa lilipo jirani na Bomani kama unaelekea Barabara ya Mbeya–Tunduma likitazamana na Kituo cha Polisi.

Mwanakwetu anayesema haya kwa masikitiko makubwa maana Disemba 14, 2022 alipigiwa simu ya mwanahabari Frank Kashonde na kumjulisha kufariki kwa Joachim Kapembe ambaye alifanya naye kazi kwa karibu mno.

Joachim Kapembe alikuwa Mmakonde mwenye asili ya mikoa ya kusini mwa Tanzania lakini mzaliwa wa Tanga wazazi wake wakienda kufanya kazi katika mashamba ya mkonge enzi hizo. Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe, amina.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news