NA ADELADIUS MAKWEGA
WAKATI fulani mwanakwetu alikuwepo katika Kitongoji cha Kidunda, Kijiji cha Michungwani wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.
Akiwa hapo walikuwepo watoto wake wa kiume na wa kike. Siku hiyo ilikuwa likizo kazi ziligawanywa, wengine wakilima na mabinti wakifanya kazi za jikoni ili wale waliokuwa shambani muda wa chakula ukifika wale kwa wakati.
Kazi ya kupika haikuwa nyepesi, kwani ililingana fika na wale waliokuwa shambani kwa kuwa waliokota kuni, kuchanja na kupika chakula cha watu wengi.
Washambani walifanya kazi zao na kumaliza na wakupika waliivisha na kutenga chakula hicho katika makundi manne; wanaume, wanawake, watoto na chakula cha wanyama na kila kundi lilianza kuyatupa mawe pangoni.
Kundi la wanaume ambalo mwanakwetu alikuwepo walipoanza tu kula kukawa na miguno mmmm, mmmm na mmmm.Mwanakwetu alimega ugali na kulichovya tonge katika mboga na kuliweka kinywani mwake aligundua siri ya miguno hiyo, “Jamani chakula chenu kinakuwa kama makapi, hakina chumvi tunaombeni chumvi.”
Katika kundi hili kila mmoja akasema ni kweli, mwanakwetu akauliza mbona mlikuwa mnaguna tu? Kijana mmoja alisema, “Nyumba za watu zina miiko yake, pengine wangine wamekwenda kwa waganga wameambiwa wale chakula kisicho na chumvi tu.”
Aliyepika alisikia maneno haya ya mwanakwetu, kwa hiyo alipotoka kuwapa chumvi wanaume watoto nao waliomba chumvi hiyo. Malalamiko hayakusikika katika makundi mawili wanyama na wanawake, lakini hawa wanawake wenyewe ndiyo wapishi.
Malalamiko ya wanawake hayakusikika maana wao wapo jikoni wanaweza wakapika tena, wanaweza wakaunga tena maana ya jikoni ni ya jikoni na hiyo ndiyo raha ya kuwa mpishi na raha kuwa mekoni.
Hivi wajikoni aibuke na kusema maharagwe haya hayana chumvi! Ataulizwa wewe si huko jikoni na umepika mwenyewe kazi kwako fanya uwezalo.
Mwanakwetu aliwaonea huruma wanyama wake mbwa na paka maana wao hawakujaliwa uwezo wa kulalamikia hilo na alibaini kuwa kulalamika si uwezo wa viumbe hai wote bali kwa binadamu lakini nalo hilo huyu binadamu linategemea mambo mengi yanayamzunguka hapo alipo.
Makundi yote manne yalipomaliza kula tu kijana mmoja akawaambia wale mabinti waliopika kuwa mnapokuwa mnapika chakula cha watu wengi mjitahidi sana kutambia kiasi cha chumvi kinachotosha, hapo usiweke chumvi nyingi na wala usiweke chumvi kidogo weka chumvi ya wastani.
“Chumvi mekoni na maana chumvi ya jamvini hainogi, mtaachwa na waume zenu mkiendelea na tabia hii dada zangu.Hamjipikii wenyewe, mnapikia wengi.”
Mpishi inawezekana unashida ya ulimi wako kuonja chumvi vizuri, hilo lisikupe tabu chagua mtu mmoja miongoni mwa wanaokula muite aonje chumvi hiyo wakati unapika ili kuondoa malalamiko, kijana huyu aliendelea kuwananga binti wa mwanakwetu.
Watu wote walipumzika kwa saa moja alafu kurejea kazini. Wakiwa kazini mwanakwetu alimuuliza yule kijana akisema mbona leo umelalamikia sana kuhusu chumvi? Kijana huyu akajibu kuwa kabla ya kurudi nyumbani kwao Michungwani aliwahi kufanya kazi Dar es Salaam katika makazi ya familia moja.
Hapo chakula kilikuwa kinapikwa na mama mwenye nyumba ambaye yeye hatumii kabisa chakula chenye chumvi,. Chakula kikipikwa chumvi inawekewa mezani kwa kila mmoja katika sahani yake.
Jambo hilo lilimsumbua sana na kusema alitamani kuliweka wazi, lakini taya lake lilipewa mzigo wa kilo hamsini na kushindwa kutamka hilo huku akiumia nalo moyoni.
Suluhu ya hilo kwake siku alizokuwa na pesa alikuwa anatoka anakwenda kula kwa Mama Ntilie. Sasa mwanakwetu huyu yeye ni kibarua hiyo pesa ya kula mgahawani kila siku anaitoa wapi?.
“Pale tulikuwa tunatamani apike binti wa kazi angalau aweze kutuungia mboga yetu chumvi ikiwa mekoni, hilo kumuomba mama mwenye nyumba ilikuwa ngumu sana. Tulibaki nalo moyoni tu, huku mama mwenye nyumba mwenyewe kila siku yupo jikoni akipenda sana kupika, nani wa kumbandua jikoni ? Nyumba yake, pesa anatoa yeye, jiko lake, mkaa ananunua yeye. Unalo la kulisema hapo ?”.
Baba wa mji huu alikuwa na wake wawili kwa hiyo alikuwa akionekana mara chache na kama angekuwa yupo kila siku ingekuwa nyepesi kuliona hilo na kulisemea, lakini moyoni mwa huyu kijana alisema kuwa hata baba wa mji huo angekuwepo kila siku je pengine kupikiwa kisicho na chumvi ndicho kilichomshawishi amuoe huyu mama? Kubwa ilikuwa kukaa kimya tu au kwa majaliwa ya Mungu mama huyu mwenyewe atambue hilo.
Kila siku iliyokwenda kwa Mungu iliendelea miguno ya moyoni tu kwa wafanyakazi wa nyumba hii.
Kununua kila siku chakula alishindwa na miaka ilisonga huku akiwa hana lolote alilofanya muda aliofanya kazi hapo maana pesa yote ilimalizikia katika kununua chakula kilichoungwa chumvi vizuri kwa Mama Ntilie, hivyo alikata shauri kuondoka, alimuaga mama huyu na kurudi zake Handeni na ndipo alipokutana na mwanakwetu siku hiyo.
Mwanakwetu na ndugu hawa walifanya kazi siku hiyo na kisha kila mmoja kulipwa haki yake na kurudi majumbani mwao.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
NB-Mwanakwetu anakutakia heri ya Noeli na Mwaka Mpya 2023.