Dhana ya Afya Moja kushirikisha kundi la wenye ulemavu

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Taasisi ya Tanzania Mission for Illiteracy and Poverty Alleviation (TAMIPA), Bw. Martin Kidudu amesema kundi la wenye ulemavu litaendelea kushirikishwa katika mipango ya dhana ya Afya Moja nchini kwa kutambua michango yao katika jamii.
Ametoa kauli hiyo wakati akitoa wasilisho kuhusu mradi unaohamasisha kuongeza nafasi ya wenye mahitaji maalumu (Wenye ulemavu) katika dhana ya afya shirikishi (One Health) na kupambana dhidi ya usugu wa vimelea vya magonjwa (Antimicrobial Resistanceake) wakati wa Mkutano wa Maafisa Viungo wa Afya Moja walipokutana kwa ajili ya kufanya Tathimini ya Utekelezaji wa shughuli zao kwa mwaka 2022 walipokutana mkoani Morogoro. 

Amesema kundi la watu wenye ulemavu linapaswa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia michango waliyonayo katika jamii huku akieleza namna Taasisi yake ilivyolifikia kundi hilo.

"Kwa kutambua michango ya watu wenye ulemavu tutaendelea kuwashirikisha ili wapewe nafasi ya kutoa michango yao katika jamii na maendeleo ya nchi,"alisisitiza.

Alifafanua kuwa, kundi hili ni sehemu muhimu katika jamii hivyo waendelee kuhusishwa katika mipango na mikakati mbalimbali kama inakifanyika kwa watu wengine.

"Licha ya ulemavu walionao watu hawa wana mchango mkubwa sana katika jamii. Dunia kupitia Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs) 2030 pamoja na kauli mbiu ya WAAW 2022- Fighting AMR together calls for 'No One Left behind’ambapo falsafa hii inaleta chachu ya kutoacha kundi lolote nyuma na zinahimiza kutambua na kuthamini makundi yote,” alieleza Kidudu.

Aliongezea kuwa, katika wiki ya uelewa wa vimelea vya magonjwa (World Antibiotic Awareness Week- WAAW) mwaka 2022 walifanikiwa kuwafikia watu wenye ulemavu 304 ambapo kati yao 204 ni mwenye ulemavu wa kusikia, 98 wenye ulemavu wa kuona pamoja na 56 wenye mahitaji maalum zaidi ya moja.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa jitihada za kuhakikisha inaboresha mazingira ya watu wenye mahitaji maalumu kwa kuzingatia Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 inayotambua nafasi ya watu wenye ulemavu katika kuchangia maendeleo ya nchi na inawahamasisha kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza ili kujikwamua kiuchumi.

“Kipekee naipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jitihada wanazozifanya katika utekelezaji wa dhana ya afya Moja kuwa shirikishi, nitoe rai kwa wadau kuendelea kuunga mkono jitihada hizi,"alisisitiza. 

Pamoja na hayo aliwaomba wadau kuendelea kushirikiana na Taasisi ya TAMIPA katika kuhudumia wenye mahitaji maalum.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news