NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Mashtaka nchini,DPP Sylvester Mwakitalu ametembelea Gereza Kuu la Isanga jijini Dodoma kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili Maafisa wa Magereza katika kuwatunza wafungwa pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili mahabusu.
Mkuu wa Gereza Kuu la Isanga, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Ikobela Fumbuka akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu walipotoka kuwatembelea Wafungwa na Mahabusu Wanawake waliopo katika Gereza Kuu la Isanga ambapo katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka na timu yake walipata nafasi ya kujua changamoto zinazowakabili na kuzichukua kwa lengo la kuzishughulikia. Mahabusu hao wanawake walipongeza juhudi mbalimbali za kazi zinazotekelezwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ambazo wamesema wanazifuatilia kupitia televisheni wanazoangalia wakiwa gerezani hapo.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Sylvester Mwakitalu akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma wakiwa na Maafisa Magereza walipotembelea Gereza Kuu la Isanga lililopo jijini Dodoma kwa lengo la kuwatembelea Maafisa Magereza, Mahabusu na Wafungwa ili kuwasikiliza na kukiona changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa lengo la kuzitatua ziara hiyo imefanyika jijini Dodoma leo Desemba 5, 2022.
Baadhi ya viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakiongozwa na Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi, Bw. Tumaini Kweka wakitoka katika Gereza Kuu la Isanga lililopo jijini Dodoma kuwatembelea Wafungwa na Mahabusu waliopo katika gereza ili kuwasikiliza na kuhusiana changamoto zinazowakabili. Viongozi hao wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu (hayupo pichani ) katika ziara iliyofanyika leo Desemba 5,2022.
Akizungumza baada ya kutembelea Gereza Kuu la Isanga Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kuwa lengo la kutembelea wafungwa na mahabusu ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa misingi ya sheria na kanuni zake.

Amesema, miongoni mwa changamoto ambazo amezipokea katika ziara yake ambazo mahabusu wamezieleza ni suala zima la ucheleweshwaji wa kesi na kuchelewa kwa upelelezi ambapo ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kuzishughulikia changamoto hizo kwa kuhakikisha kuwa wameshasajili Hati za Mashtaka Mahakama Kuu ambazo hivi sasa zipo katika mchakato wa kusikilizwa.


