FEI TOTO TUMSAMEHE WANAYANGA WENZANGU

NA ELIUS NDABILA

NDUGU zangu Wanayanga ninaomba TUMSAMEHE sana Feisal Salum Abdalla (Fei Toto).
Kumekuwa na mjadala wa siku kadhaa juu ya Fei Toto ambaye tuliambiwa amevunja mkataba na Yanga illegally.

Kumekuwa na mijadala yenye hisia tofauti. Taarifa ambazo si rasmi zinasema Fei Toto amerejea Yanga baada ya kugundua makosa yake.

Mimi nilikuwa sehemu ya tuliokwazwa na njia aliyotaka kutumia FEI TOTO kuikimbia Yanga. Kwenda Azam FC haikuwa issue, kwani alifuata masilahi, lakini njia aliyotumia haikuwa sahihi.

Wakati ninatafakari namna ya kuwaomba Wanayanga kumsamehe na kuacha maisha mengine yaendelee nikakumbuka neno Moja kutoka kwenye Biblia. Neno ambalo linatoka Kitabu cha YOHANA 8:3-11.

Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini.

Wakamsimamisha katikati ya watu wote. Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini. Katika sheria, Musa ametuamuru kuwapiga mawe wanawake waliokamatwa wakizini, mpaka wafe. Sasa wewe wasemaje?” Walimuuliza hivi kwa kumtega, kusudi wapate sababu ya kumshtaki.

Lakini Yesu akainama chini akaanza kuandika kwa kidole chake mavumbini. Walipoendelea kumuulizauliza akainuka, akawaambia, “Asiyekuwa na dhambi kati yenu awe wa kwanza kumtupia jiwe.”

Akainama tena akaendelea kuandika chini. Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, akianza mkubwa wao.

Yesu akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama pale walipomwacha.Yesu akasimama akamwuliza, “Mama, wale waliokuwa wanakushtaki wako wapi?.

Hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?” Yule mwanamke akajibu, “Hakuna Bwana.” Yesu akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Unaweza kwenda, lakini usitende dhambi tena.”

Wanayanga wenzangu, nani hajawahi kukosea? Nani angepewa fedha tunayoambiwa Azam walimpa Fei Toto tena kwa umri angekumbuka kutumia njia sahihi kuondoka huku akijua nitazuiwa?.

Fei Toto ni kijana wetu tangu maisha yake ya utoto. Haya yanathibitishwa kwenye interview mbalimbali ambazo vyombo vya habari vimekuwa vikiifanyia familia yake.

Pamoja na mapenzi yake Yanga, lakini fedha ina nafasi kubwa, kwani maisha ya mpira ni mafupi. Binadamu ameumbiwa kukosea, njoo TUMSAMEHE maisha yaendelee.

Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa Mbinguni atawasamehe ninyi.

Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.Ni agizo la MUNGU kuwasamehe watu wanaokukosea.

Usipowasamehe huwezi kuingia uzima wa milele hata kama unajiona ni mtakatifu kiasi gani.

Usikupokuwa mtu wa kusamehe watu hakika hata wewe mwenyewe hautasamehewa na MUNGU.

Ni MUNGU ametuagiza tuwe watu wa msamaha hivyo ni lazima tutekeleze agizo la MUNGU.Usiposamehe watu wewe ni muuaji na wauaji hawana sehemu katika ufalme wa MUNGU wasipotubu na kuacha dhambi hiyo.

Tuanze safari upya,
Elius Ndabila (Ibaba Ileje)
0768239284

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news