Gwiji wa soka duniani, Pele afariki dunia

NA DIRAMAKINI

GWIJI wa soka duniani Edison Arantes do Nascimento (Pele) ambaye ni raia wa Brazil amefariki leo Desemba 29, 2022.

Pele ndiye anayechukuliwa kuwa mchezaji bora zaidi wa soka ambaye ujuzi wake uwanjani ulisaidia kuutangaza kama mchezo mzuri,amefariki leo kufuatia mapambano ya mwaka mzima dhidi ya saratani ya utumbo.

Binti yake, Kely Nascimento amethibitisha kifo hicho kwenye Instagram yake,"Kila kitu tulicho nacho ni kwa sababu yako. Tunakupenda sana. Pumzika kwa amani," Kely Nascimento aliandika.

Nyota huyo ambaye alizaliwa Oktoba 23, 1940 amefariki akiwa na umri wa miaka 82 katika Hospitali ya Israeli ya Albert Einstein huko São Paulo, Brazil.

Pele anahesabiwa na wengi wakiwemo wachambuzi mahiri wa soka duniani na mashabiki, kuwa mchezaji bora zaidi wa wakati wote.

Wakati wa uhai wake, kabla ya kustaafu soka, alicheza kama mshambuliaji wa kati. Aliisaidia Brazil kutwaa Kombe la Dunia 1958, 1962 na baadaye tena mwaka 1970.

Gwiji huyo aliweka rekodi mwaka 1958 ya kuwa mchezaji mdogo kuliko wote duniani kucheza katika fainali ya Kombe la Dunia alipocheza akiwa na umri wa miaka 17. Alivuma sana katika miaka ya 1970 duniani kote.

Mwaka 1999 alichaguliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuwa mchezaji bora wa karne. Kwa mujibu wa FIFA, Pele alikuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kufunga magoli 1281 kati ya mechi 1363.

Pia ana wastani wa goli moja kwa kila mechi katika uchezaji wake wote. Katika kipindi cha uchezaji wake alikuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi duniani.

Nyota huyo alianza kuichezea Santos akiwa na umri wa miaka 15 na timu ya taifa ya Brazil akiwa na miaka 16. Katika ngazi za kimataifa alishinda Kombe la Dunia mara tatu akiwa ni mchezaji wa pekee kufanya hivyo.

Ni mchezaji wa Kibrazil anayeongoza kwa magoli mengi zaidi kwa kufunga magoli 77 kwenye mechi 92.Kwenye ngazi ya klabu ni mfungaji bora wa muda wote katika klabu ya Santos, na aliisaidia kubeba taji la Copa Libertadores kwa miaka ya 1962 na 1963.

Kwa mchezo wake wa haraka,chenga zake na magoli yake ya kushangaza yalimpa umaarufu duniani kote.Tangu alipostaafu mwaka 1977,Pele kabla ya umauti kumkuta amekuwa balozi wa mpira wa miguu duniani.

Wakati wa uhai wake, Pele alikuwa na uwezo wa kuupiga mpira kwa mguu wowote ili kuwazidi ujanja wapinzani wake uwanjani.

Akiwa bila mpira kwa muda mrefu hurudi nyuma na kufanya kazi ya kukabana kusawazisha mipira na kutumia uwezo wake wa kupiga pasi kwa kutoa pasi za zinazozaa mabao na kutumia uwezo wake wa kukokota mpira kuwapita wapinzani.

Brazil wanamuheshimu kama shujaa wa taifa kwa mchango wake wa kisoka na sera zilizosaidia katika kupunguza umaskini katika nchi hiyo.

Katika uchezaji wake na mpaka kustaafu amepokea tuzo nyingi za timu na za binafsi kwa uwezo wake anapokuwa uwanjani na uvunjaji rekodi wake.

Pelé alizaliwa mjini Três Corações, Minas Gerais, Brazil na ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Fluminense Dondinho (mtoto wa João Ramos do Nascimento) na Celeste Arantes.

Ni mkubwa kati ya watoto wawili. Alipewa jina la shujaa wa Kimarekani Thomas Edison. Wazazi wake waliamua kuitoa herufi "i" na kumuita "Edson",lakini kulikuwa na makosa kwenye cheti chake cha kuzaliwa kusababisha litumike jina la "Edison" badala ya "Edson".

Familia yake walimpa jina la "Dico". Alipewa jina la "Pelé" alipokuwa shule inaposemekana kuwa alishindwa kutamka jina la golikipa wa timu ya Vasco Da Gama anayeitwa Bilé,alivyozidi kulitamka ndivyo alivyozidi kuchapia.
Pelé aliwahi kusema hakujua maana ya jina hilo wala marafiki zake waliompa jina hilo.Lakini jina hilo lilitokana na jina la Bilé, lakini kwa Kiebrania maana yake ni maajabu, lakini jina halina maana yoyote kwa Kireno.

Pelé alikulia katika hali ya umaskini huko Bauru kwenye mji wa Paulo.Alijikusanyia fedha kidogo alipofanya kazi kwenye duka la chai.

Alfundishwa kucheza mpira wa miguu na baba yake, lakini hakuweza mara acheze na soksi iliyojazwa na magazeti au magada ya mapera huku akifunga na kamba.

Amechezea klabu nyingi za vijana kama Sete de Setembro, Canto do Rio, São Paulinho, na Amériquinha. Pelé aliisaidia Bauru Athletic Club klabu ya vijana (ikifundishwa na Waldemar de Brito) kushinda mataji mawili ya mashindano ya klabu za vijana za São Paulo.Pelé alishindana mashindano ya mpira wa miguu ya ndani ya chumba ambapo aliisaidia timu yake ya Bauru.

Pelé aliwahi kukiri kuwa mashindiano hayo yana changamoto kubwa,alisema kuwa mchezo huo ulikuwa wa haraka kidogo kuliko mpira wa miguu wa kwenye nyasi na kwamba mchezo huo ulihitaji uwezo mkubwa wa kufikiri haraka kwa kuwa kila watu wanakuwa karibu karibu ndani ya uwanja.

Pelé anauheshimu sana mchezo huo kwa kuwa ulimpa uwezo mkubwa wa kufikiri papo kwa papo anapokuwa uwanjani. (Mashirika)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news